Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atimiza miaka 90 | Matukio ya Afrika | DW | 21.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atimiza miaka 90

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anasherehekea hii leo (21.02.2014) miaka 90 ya kuzaliwa kwake. Katika nchi za Magharibi anatajwa kuwa "muimla katili" barani Afrika lakini bado kuna wanaomshangiria

Robert Mugabe

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Je, Robert Mugabe ni muimla? Baffour Ankomah anayemjua binafsi rais huyo wa Zimbabwe anahisi huo ni upuuzi mtupu. Anasema "Ukisoma vyombo vya habari vya Magharibi utafikiri bwana huyu anawala wananchi wake kama chakula cha asubuhi, mchana na usiku. Lakini mtu anapojuana naye, unakuta kuwa ni mtu mwengine kabisa."

Anasimulia mhariri mkuu huyo wa jarida la New Africa linalochapishwa mjini London. "Cha kuvutia zaidi ni moyo wake mzuri na ukarimu wake", anaelezea kwa fahari Ankomah.

Wengine wamwita shujaa wa uhuru

Amtsvereidigung Robert Mugabe 22.08.2013

Rais Mugabe akila kiapo

Mwandishi habari huyo wa kutoka Ghana na jarida lake ni miongoni mwa mashabiki wa Mugabe katika jukwaa la vyombo vya habari vya kimataifa. Wao wanamwangalia muimla huyo, ambaye Umoja wa Ulaya, miongoni mwa taasisi nyenginezo, umemwekeya vikwazo kwa sababu ya kuvunja vibaya sana haki za binaadamu, kuwa bado ni shujaa wa uhuru.

Mugabe ameupata umashuhuri wake miongoni mwa viongozi wengine wa Afrika kutokana na mbinu na werevu wake wa kisiasa. Akiwa mpiganaji wa chini kwa chini dhidi ya utawala wa Wazungu wachache katika ile iliyokuwa ikijulikana zamani kama Rhodesia, alikuwa na maingiliano na wanaharakati kadhaa wa Kiafrika waliokuwa wakipigania uhuru. Alikuwa karibu sana na kwa muda mrefu na chama cha ukombozi wa Afrika Kusini, African National Congress - ANC, na baadhi ya wakati aliwahi pia kuishi uhamishoni nchini Tanzania na Msumbiji. Wengi kati ya wanaharakati wenzake wa zamani wamegeuka kuwa marais au wanasiasa mashuhuri na wote wanamuunga mkono muimla huyo wa Harare. Anasema Andrea Jeska, mwandishi habari wa kijerumani aliyeandika kitabu kuhusu ZImbabwe, "Nakumbuka niliwahi kumuuliza rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano kwa nini mwanademokrasia kama yeye anaendeleza urafiki na mtu kama Robert Mugabe. Alikasirika na kuniambia nnamchukulia yeye kuwa ni mtu wa aina gani hata amwache mkono rafiki yake wakati anakumbwa na shida."

Baadhi ya matamshi ya Mugabe yafurahisha baadhi ya Waafrika

Simbabwe Obst- und Gemüsemarkt in Jambanja

Raia wa Zimbabwe wakiwa kazika soko la mboga la Jambanja

Hata miongoni mwa wakaazi wa baadhi ya mataifa ya Afrika matamshi makali ya Mugabe dhidi ya nchi za Magharibi yanawavutia. Anapokosoa ushawishi wa nchi za Magharibi na kudai Waafrika wajiamulie wenyewe kuhusu mustakbali wa nchi zao na utajiri wao wa mali ghafi, matamshi hayo yanawaamsha wengi wa Waafrika kwa sababu umaskini na ugavi usio wa haki wa utajiri unaotokana na mali ghafi baada ya miongo kadhaa ya enzi za ukoloni ni mambo yanayoshuhudiwa mpaka leo katika nchi nyingi za Afrika.

Mfano wa Namibia ilipojipatia uhuru mwaka 1990 kutoka Afrika kusini, takribani nusu ya ardhi ya kilimo imekuwa ikimilikiwa na wakulima 3,500 tu wenye asili ya Kizungu. Wanamibia weusi hawakuwa na nafasi yoyote ya kumiliki ardhi si chini ya enzi za ukoloni wa Ujerumani na wala si pale ilipovamiwa na kukaliwa na Afrika Kusini.

Hali sawa na hiyo inakutikana pia nchini Afrika Kusini. Na ingawa hivi sasa inatumika sheria ya mageuzi ya kumliki ardhi, lakini Waafrika Kusini walio wengi hawana fedha kuweza kununua ardhi. Yote hayo yanachangia kumfanya Mugabe asifiwe barani Afrika.

Mwandishi: Daniel Pelz/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza