1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ramaphosa akutwa na COVID-19

Grace Kabogo
13 Desemba 2021

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa anapatiwa matibabu baada ya kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 baada ya kujisikia vibaya siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/44ApD
Deutschland | G20 | Compact with Africa meeting in Berlin | Cyril Ramaphosa
Picha: Tobias Schwarz/REUTERS

Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imesema Ramaphosa ambaye amepata chanjo kamili ya virusi vya corona, alianza kujisikia vibaya baada ya kuondoka katika Ibada ya kitaifa ya kumbukumbu ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, FW de Klerk mjini Cape Town, mapema Jumapili. Taarifa hiyo imeeleza kuwa kiongozi huyo anaendelea vizuri, lakini yuko chini ya uangalizi wa Idara ya Afya ya Jeshi la Afrika Kusini.

Ramaphosa mwenye umri wa miaka 69, amekabidhi majukumu yake kwa Makamu wa Rais, David Mabuza kwa wiki yote hii. Hata hivyo, taarifa hiyo haijaeleza iwapo Ramaphosa ameambukizwa aina mpya ya kirusi cha Omicron. Wiki iliyopita, Ramaphosa alizuru nchi nne za Afrika Magharibi.

Ujumbe wa Ramaphosa na vipimo vya COVID-19

Yeye na ujumbe wake walipimwa COVID-19 katika kila nchi walipowasili na baadhi ya maafisa walikutwa na virusi vya corona nchini Nigeria na walirejea mara moja Afrika Kusini. Wakati wote wa ziara hiyo, Ramaphosa hakukutwa na virusi vya corona. Kiongozi huyo alirejea Afrika Kusini Desemba 8, akitokea Senegal.

Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani, WHO na Benki ya Dunia zimesema zaidi ya watu nusu bilioni ulimwenguni walikumbwa na umasikini uliokitihiri mwaka uliopita kutokana na kuongezeka kwa gharama za afya wakati wa janga la virusi vya corona. Mashirika hayo yamesema kuathirika kwa huduma za afya wakati wa janga hilo kumechochea mzozo mkubwa zaidi wa kiuchumi duniani tangu miaka ya 1930, hali iliyosababisha kuongezeka kwa gharama za huduma za afya. Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema serikali zote zinapaswa kuhakikisha wananchi wao wanapata huduma za afya bila ya kuwa na hofu ya atahri za kifedha.

Großbritannien London | Ansprache Boris Johnson zu Omicron
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson Picha: Kirsty O'Connor/AFP/Getty Images

Ama kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema nchi hiyo inakabiliwa na wimbi kubwa la aina mpya ya kirusi cha Omicron. Johnson amesema dozi mbili za chanjo hazitoshi kukabiliana na kirusi hicho.

''Lakini habari njema ni kwamba wanasayansi wetu wana uhakika kuwa dozi ya tatu, inaweza kuinua kiwango chetu cha kujilinda. Kila mtu anayestahili mwenye miaka 18 na zaidi nchini Uingereza atakuwa na nafasi ya kupata chanjo ya nyongeza kabla ya Mwaka Mpya,'' alifafanua Johnson.

Chanjo kwa watoto wa miaka 5-11

Huku hayo yakijiri jimbo la Berlin litaungana na majimbo mengine ya Ujerumani kuanza kutoa chanjo ya virusi vya corona kwa watoto kuanzia umri wa miaka mitano hadi 11. Maafisa wa afya wa Berlin wamesema watoto hao watastahili kuanza kupata chanjo ya Pfizer na BioNTech wiki hii mjini Berlin. Chanjo hizo zitatolewa katika vituo vya chanjo vilivyowekwa kwenye shule, ofisi za madaktari na hata kwenye makumbusho ya taifa.

Majimbo mengine ya Ujerumani yatakayoanza kutoa chanjo kwa watoto katika siku zijazo ni pamoja na North Rhine-Westphalia, Hamburg na Bavaria. Aidha, taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza Ujerumani,Robert Koch Jumatatu imerekodi visa vipya 21,743 vya corona na vifo 118.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amekanusha taarifa iliyoandikwa na gazeti la Bild kwamba chanjo zimeligawa taifa hilo. Akizungumza katika mahojiano, Scholz amesema kuwa na maoni tofauti hakumaanishi ni kugawanyika. Amesema yeye ni kansela pia wa wale ambao hawajachanjwa, na angependa kuwashauri kuwa chanjo ina maana na ni muhimu.

(AFP, AP, DPA, DW, Reuters)