1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Rais Putin amuondoa Sergei Shoigu kama waziri wa ulinzi

13 Mei 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin amemuondoa Sergei Shoigu kama waziri wa ulinzi katika mabadiliko aliyoyafanya ya Baraza la mawaziri wakati anapoanza awamu yake ya tano madarakani.

https://p.dw.com/p/4flgX
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na Waziri wa Ulinzi anayeondoka Sergei Shoigu
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na Waziri wa Ulinzi anayeondoka Sergei ShoiguPicha: Mikhail Klimentye/REUTERS

Ikulu ya Kremlin imeeleza kuwa Shoigu badala yake ameteuliwa kuwa katibu wa Baraza la Usalama la Urusi.

Rais Putin amemteua Andrei Belousov, naibu waziri mkuu wa zamani ambaye amebobea katika masuala ya uchumi, kuwa waziri mpya wa ulinzi.

Belousov hata hivyo atahitaji kuidhinishwa na bunge.

Soma pia: Urusi yadai kukamata vijiji sita mashariki mwa Ukraine

Kwa mujibu wa sheria ya Urusi, Baraza lote la Mawaziri lilijiuzulu siku ya Jumanne baada ya kuapishwa kwa Putin japo mawaziri wengi walitarajiwa kuhifadhi nafasi zao.

Shoigu aliteuliwa kuhudumu kama waziri wa ulinzi mwaka 2012, miaka miwili kabla ya Urusi kulinyakua jimbo la Ukraine la Crimea.

Mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri yanatokea katikati ya mashambulizi yanayofanywa na Urusi katika mkoa wa Kharkiv, kaskazini mashariki mwa Ukraine ambapo maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.