Rais Vladimir Putin amesema Urusi italenga kuongeza biashara na mataifa ya Afrika maradufu katika muda wa miaka mitano ijayo, wakati akifungua mkutano wa kilele wenye lengo la kufufua mahusiano ya Moscow na bara hilo.
Rais wa Urusi amekuwa mwenyeji wa viongozi kadhaa wa mataifa ya Afrika leo kwa mkutano wa kwanza wa kilele kati ya Urusi na bara la Afrika, na kuakisi msukumo mpya wa Urusi kupanua ushawishi wake katika bara hilo na kusema kuna nafasi kubwa sana kwa ukuaji wa uhusiano huo.
Wenyeji wa mkutano kati ya Urusi na Afrika , marais Vladimir Putin wa Urusi (Kushoto) na Abdel Fattah el-Sissi wa Misri mjini Sochi.
Putin na rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi ni wenyeji wa mkutano huo wa siku mbili unaoahudhuriwa na viongozi 43 wa mataifa 54 ya bara hilo, ambapo mataifa mengine yanawakilishwa na maafisa waandamizi.
Putin amesema biashara inayofanywa na Urusi kwa mwaka pamoja na mataifa ya Afrika ilipanda maradufu katika miaka mitano iliyopita na kupindukia dola bilioni 20.
Amedokeza kwamba, "ni wazi kwamba haitoshi" na kuelezea nia yake kwamba biashara hiyo itaongezeka tena maradufu , "kwa wastani" katika miaka mingine minne ama mitano.
El-Sissi amehimiza makampuni ya Urusi kupanua uwekezaji wao katika bara la Afrika. "Kuna fursa muhimu kwa hilo hivi sasa," amesema.
Urusi na ushawishi katika Afrika
Urusi imefanyakazi kwa mbinu sahihi katika miaka ya hivi karibuni kupanua ushawishi wake katika bara la Afrika, ikichukua fursa ya kupungua kwa hamasa ya Marekani katika bara hilo chini ya utawala wa rais Donald Trump. Akichangia katika mjadala kuhusu uhusiano kati ya Afrika na Urusi rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa alisema.
"Uhusiano wetu haukuanza jana. Ulikuwapo kwa miaka mingi na umekuwa uhusiano uliotengenezwa katika mapambano. Na kwa njia nyingi, Afrika kusini, Afrika kusini iliyo huru, iko hivyo leo kutokana na sababu ya msaada tulioupata kutoka kawa watu wa Urusi."
Shirika la Urusi la uchunguzi wa miamba na ardhi limetia saini makubaliano na Sudan kusini , Rwanda na Guinea kutafuta maliasili za mafuta na makaa ya mawe. Putin pia alikutana na viongozi kadhaa wa Afrika kujadili kuhusu uwezekano wa miradi kadhaa. Putin alisema.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria (kushoto) na Cyril Ramaphosa (kulia9 wa Afrika kusini wamekutana tena mjini Sochi katika mkutano kati ya Urusi na Afrika.
"Urusi , kama kiongozi wa dunia katika nyanja ya nishati ya nyuklia na uzalishaji wa mafuta ya nyuklia, pamoja na Namibia, ambayo ni mtoaji mkuu wa madini ya urani, zunaweza kuanzisha ushirikiano wa karibu na kuwa washirika wazuri."
Putin amempongeza waziri mkuu wa Ethipia Abiy Ahmed kwa kushinda tuzo ya amani ya Nobel mapema mwezi huu, akisifu juhudi zake za kuleta amani na nchi hasimu wa siku nyingi Eritrea.