1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama ziarani Saudi Arabia

28 Machi 2014

Rais Barack Obama wa Marekani leo anaondoka Ulaya baada ya kukamilisha ziara yake ya siku nne barani humo na sasa anaelekea Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/1BXi8
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: Reuters

Ziara ya rais Obama katika taifa hilo la Kifalme inatarajiwa kutuwama zaidi katika kuiangalia mizozo ya Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na suala la Nyuklia la Iran.

Rais Obama atakutana na Mfalme Abdullah na anatarajiwa kuihakikishia Saudi Arabia nchi ambayo ni mshirika wa Marekani kwamba ingawa majeshi ya Marekani yameondolewa Iraq na Afghanistan pamoja na kushiriki nchi hiyo katika mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, Marekani haijautenga ulimwengu wa Kiarabu.

Saudia ina hofu kuhusu Iran

Maafisa wa Ikulu ya Marekani pamoja na wataalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, wamesema kuwa hofu kubwa ya utawala wa Saudi Arabia, ni mpango wa nyuklia wa Iran na hasa nchi hiyo inavyoiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria. Aidha, Saudi Arabia ina wasiwasi kuhusu mpango wa serikali ya Iran kuwa na maeneo ya kuchimba mafuta nchini humo pamoja na Bahrain.

Mshauri wa Rais Obama katika masuala ya usalama wa taifa, Ben Rhodes, amesema mazungumzo ya viongozi hao wawili yatahusu usalama katika eneo la Ghuba, uungaji mkono wa Marekani kwa waasi wa Syria, mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati pamoja na mazungumzo kuhusu mzozo wa nyuklia wa Iran.

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia
Mfalme Abdullah wa Saudi ArabiaPicha: Reuters

Rhodes amesema mazungumzo kati ya Rais Obama na Mfalme Abdullah, yanafanyika baada ya Saudi Arabia kukataa kumpa Visa mkuu wa gazeti la Washington la The Jerusalem Post, aliyetaka kuripoti kuhusu ziara ya Rais Obama.

Obama kukutana pia na Mwanamfalme wa Abu Dhabi

Kabla ya mkutano wake na Mfalme Abdullah, Rais Obama atakutana na Mwana Mfalme Mohamed bin Zayed wa Abu Dhabi, nchi ambayo ni mshirika wa karibu wa Saudi Arabia.

Wasiwasi wa Saudi Arabia utatawala mazungumzo ya viongozi hao wawili, siku chache baada ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kumalizika huko Kuwait, huku wajumbe wakiwa wana misimamo tofauti.

Wajumbe hao waligawanyika kutokana na suala la wapinzani gani wa Syria waungwe mkono. Mvutano huo uko kati ya Saudi Arabia na Qatar. Saudi Arabia na washirika wake, wanaishutumu Qatar kwa kuwapatia silaha wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu wanaopigana katika vita vya Syria.

Ziara ya Rais Obama barani Ulaya, iligusia zaidi mzozo wa Ukraine na Urusi kuhusu jimbo la Crimea, usalama wa nyuklia pamoja na kukutana kwa mara ya kwanza kabisa na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis.

Katika ziara yake hiyo, Rais Obama alielezea furaha yake ya kukutana na Papa Francis, huku akimsifu kwa huruma aliyo nayo na jinsi anavoishi na kutenda kulingana na Injili anayoihubiri.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu