Rais Obama ataka ulimwengu usio na silaha za nyuklia | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Obama ataka ulimwengu usio na silaha za nyuklia

Hotuba ya kwanza ya hadharani ya rais Obama barani Ulaya

default

Rais wa Marekani Barack Obama akihutubia maelfu ya watu mjini Pague

Rais wa Marekani Barack Obama ametoa hotuba yake ya kwanza hadharani barani Ulaya huko mjini Prague nchini Jamhuri ya Cheki, tangu alipoingia madarakani. Mada kuu ya hotuba yake hiyo ilikuwa kuangamiza silaha za nyuklia duniani na ndoto ya kuwa na ulimwengu usio na silaha za nyuklia.

Ndio anaweza! Barack Obama pengine ndiye mtu pekee duniani anayeweza kuitisha kuangamizwa kwa silaha za nyuklia bila kuchekwa. Alipokuwa mjini Prague katika Jamhuri ya Cheki hapo jana, rais Obama alizungumzia kuhusu mpango wake wa kuangamiza silaha za nyuklia na kuachana na utengenezaji wa silaha hizo.

Jaribio la roketi lililofanywa na Korea Kaskazini hapo jana ni mfano halisi ambao rais Obama ameutumia kusisitiza umuhimu wa kupambana na silaha za nyuklia. Amesema kwamba Marekani itaongoza juhudi za kuhakikisha ulimwengu una amani. Jukumu la kufanya mazungumzo ambalo rais Obama analizungumzia, ni wazo linalokubalika. Marekani ndio nchi pekee inayomiliki nyuklia ambayo imeshawahi kutumia bomu la nyuklia. Rais Obama anasisitiza bomu la nyuklia halipaswi kutumiwa tena.

Je hotuba ya rais Obama iliyosubiriwa kwa hamu na ghamu ilikuwa wito wa kumalizika kwa machafuko ya aina yote kama alivyofanya Yesu miaka 2000 iliyopita katika mahubiri yake ya mlimani? Hapana! Kuhusiana na swala la kuangamiza silaha za nyuklia rais Obama hawezi kujitumbukiza mzima mzima ndani ya maji, bali analazimika kuridhika na hatua chache anazoweza kuzipiga katika nchi kavu.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita rais Obama alikubaliana na mwenzake wa Urusi, Dmitry Medvedev, kuhusu kupunguza vichwa vya nyuklia katika pande zote mbili za bahari ya Atlantic. Kufikia mwaka 2012, vichwa hivyo vinatakiwa kubakia kati ya 1,700 na 2,200 badala ya idadi ya sasa ya 3,000. Hatua nyingine anazotaka kuchukua rais Obama ni kuitisha mkutano kuhusu usalama wa silaha za nyuklia nchini Marekani na kufikia wakati huo anataka pia awe ameidhinisha mkataba unaopinga kufanyika majaribio ya silaha za nyuklia.

Pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya na Urusi, rais Obama anataka kuizuia Iran isiwe taifa linalomiliki silaha za nyuklia, jambo ambalo linaonekana kuwa kibarua kigumu kutokana na tofauti zilizopo kati ya wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Pia mpango wa Marekani wa ulinzi dhidi ya makombora utakaojengwa mashariki mwa Ulaya unalenga kuzuia mashambulio kutoka kwa Iran, kama alivyothibitisha rais Obama. Hii ilikuwa mada ngumu kwa rais huyo wa Marekani mjini Prague kwani asilimia 70 ya Wachechnya wanaupinga mpango huo wa ulinzi dhidi ya makombora wa Marekani katika nchi yao.

Ukiachwa mbali ukosoaji huo wa mpango wa Marekani, ziara ya Obama imempa nafasi ya kueleza matarajio yake. Mbele ya umati wa watu 20,000 amethibitisha kwamba katu hatokubali kuwa dhaifu na kukubali kushindwa na kwamba pengine wakati akiwa bado angali hai, itawezekana kusiwe tena na ulimwengu wenye silaha za nyuklia. Hata ingawa Obama anaonekana kama masiha wa kizazi cha sasa anayependwa na watu wengi ulimwenguni kote, ukweli ni kwamba hana mamlaka mengi kiasi hicho!

Kufikia sasa hakujachukuliwa hatua yoyote na nchi zenye uwezo mkubwa duniani kufikia lengo la kuwa na ulimwengu usio na silaha za nyuklia, mbali na mipango ya mwishoni mwa miaka ya 1980 ambayo rais wa Marekani Ronald Reagan na mwenzake wa muungano wa zamani wa Sovieti, Mikhail Gorbachov, walitaka kuchukua. Iwapo mahubiri ya rais Obama mjini Prague yatatimia basi kweli atakuwa amefaulu kufanya muujiza.


Mwandishi: Susanne, Henn

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 06.04.2009
 • Mwandishi Charo Josephat/ Susanne, Henn
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HR6M
 • Tarehe 06.04.2009
 • Mwandishi Charo Josephat/ Susanne, Henn
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HR6M
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com