1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama asema Urusi inasua sua katika mgogoro wa Syria

5 Agosti 2016

Rais Barack Obama wa Marekani amesema Urusi itapaswa kuonyesha nia ya dhati katika juhudi zinazoendelea hivi sasa za kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1Jc2f
Rais wa Marekani, Barack Obama
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: Reuters/J. Ernst

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na washauri wake wa ngazi ya juu wa masuala ya usalama katika wizara ya ulinzi ya Marekani Rais Obama alisema Urusi lazima ionyeshe dhahiri nia yake ya kulisambaratisha kundi la Dola la Kiisilamu nchini Syria na kusisitiza kuwa Marekani haina imani na Rais wa Urusi Vladmir Putin katika suala hilo ingawa inafanya kila inaloweza katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo wa Syria na pia kulidhibiti kundi hilo la Dola la Kiisilamu.

" Vitendo vya moja kwa moja vya Urusi kuhusiana na mgogoro wa Syria katika siku za hivi karibuni vinaibua maswali mazito juu ya utayari wake katika kukabiliana na mgogoro huo " alisema Rais Obama baada ya kupokea taarifa kuhusiana na juhudi zinazoendelea dhidi ya kundi hilo la Dola la Kiisilamu.

Rais Obama alianisha maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiisilamu nchini Iraq na Syria baada ya kukutana na maafisa wa usalama na jeshi wa nchi hiyo.

Ataka makundi ya kigaidi yasambaratishwe

Aidha Rais Obama aliongeza kuwa kuwasambaratisha magaidi nchini Syria kutahitaji kukomeshwa kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na kutoa mwito kwa Urusi kuzidisha juhudi mnamo wakati Marekani ikiwa tayari kushirikiana kwa karibu na Urusi katika kuhakikisha kuwa hatua hiyo inafikiwa huku akiongeza kuwa hadi sasa Urusi imeshindwa kuchukua hatua zinazotakiwa na kuwa sasa ni muda muafaka kwa Urusi kuchukua hatua mathubuti ili kufanikisha malengo hayo.

US-Präsident Barack Obama
Picha: picture-alliance/dpa/C. Kleponis

Rais Obama alisema Marekani pia itapaswa ifanye kazi ya ziada katika kuhakikisha kuwa inasambaratisha mitandao ya kigaidi ikiwa ni pamoja na kuingilia mawasiliano ya intaneti yanayofanywa na makundi ya kigaidi ambayo yanaweza yakarahisisha utekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi.

Hata hivyo Rais Obama alikiri kuwa ugaidi hautamalizwa na utawala wake au utawala utakaokuja badala yake na kuwa siku zote amekuwa akiwasisitiza watendaji wake kuja na mawazo mapya ya kukabiliana na kitisho hicho.

Kundi la Dola la Kiisilamu limedai kuhusika na matukio mbalimbali ya kigaidi katika siku za hivi karibuni ikiwa ni pamoja na tukio la kigaidi la mwezi uliopita la mjini Nice nchini Ufaransa ambapo watu zaidi ya 80 waliuawa pamoja na mauaji yaliyofanywa katika kilabu ya usiku ya Orlando nchini Marekani ambapo watu 49 waliuawa.

Wakati hayo yakiendelea vikosi vya usalama vinavyopambana dhidi ya ugaidi nchini Misri vimedai kumuua kiongozi wa kundi la itikadi kali la Dola la Kiisilamu nchini humo Abu Doa'aa al- Ansary katika jimbo la Rasi ya Sinai kaskazini mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa katika ukurasa wa face book wa msemaji wa jeshi la nchi hiyo kiongozi huyo aliuawa pamoja na wanamgambo kadhaa wa kundi hilo katika operesheni iliyohusisha pia mashambulizi ya anga.

Mwandishi:Isaac Gamba/ DPAE/APE

Mhariri:Josephat Charo