1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Massachusetts Nachwahl Senatoren

Josephat Nyiro Charo20 Januari 2010

Chama cha Republican chashinda uchaguzi wa Massachussetts

https://p.dw.com/p/LbyB
Rais Barack ObamaPicha: AP

Kupitia ushindi wa mgombea wa chama cha Republican Scott Brown kuwania useneta katika jimbo la Massachussetts, chama cha Democratic kimepoteza wingi wake wa kura 60 katika baraza la seneti. Hilo ni pigo kubwa kwa rais wa Marekani Barack Obama ambaye hii leo anakamilisha mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani. Ushindi wa Mrepublican huyo yumkini utasababisha athari zaidi kwa utawala wa rais Obama.

Ni siku mbaya na ya uchungu kwa rais wa Marekani Barack Obama ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuingia madarakani. Matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Massachussetts si ya kuchukulia juu. Katika juhudi zake wakati wa dakika za mwisho za kampeni ya mgombea wa chama cha Democratic aliyewania kiti cha useneta, Martha Coakley, rais Obama alisisitiza kwamba uchaguzi katika jimbo la Massachussetts ungekuwa na athari katika siasa za kitaifa: Kwenda mbele au kurudi nyuma.

Wapiga kura wa Massachussets wameamua kurudi nyuma. Kwanza kabisa wamekwamisha mpango wa mageuzi ya mfumo wa afya. Wakiwa na kura zao 41 katika baraza la seneti, Warepulican sasa wana uwezo wa kuuvuruga mpango huo na hatimaye kuzuia usipigiwe kura. Ni ukweli ulio wazi dhahiri shahiri pia kwamba wingi wa kura wa chama cha Democratic katika baraza la seneti hautoshi kupitisha sheria. Na ukweli huu pia hauathiri kuanzia sasa mageuzi ya mfumo wa afya tu, bali pia miswada yote inayopendekeza mageuzi ambayo rais Obama ameipanga kuiwasilisha mwaka huu.

Angalau kabla kufikia uchaguzi wa bunge na wa baraza la seneti mnamo mwezi Novemba mwaka huu, ambapo chama cha Democratic kinatarajiwa kupoteza wabunge na maseneta, kulikuwa na ari ya kupiga hatua mbele katika kuleta mageuzi ya kisiasa nchini Marekani. Kipindi hiki sasa kimepata pigo kubwa.

Sheria kuhusu kuyalinda mazingira, sheria zinazosimamia utaratibu wa mabenki, sheria za uhamiaji na ajenda nzima ya rais Obama sasa imetiwa munda, ikiwa sio kutiliwa shaka kabisa. Kwa sababu seneta mpya wa jimbo la Massachussetts, Scott Brown, anajulikana sio tu kama mpinzani wa mageuzi katika mfumo wa afya, bali pia anapinga biashara ya gesi za viwanda na msamaha kwa wahamiaji.

Scott Brown gewinnt Wahl in Massachusetts Senat
Seneta wa jimbo la Massachusetts Scott BrownPicha: AP

Scott Brown anaunga mkono utumiaji wa mfumo wa kuwahoji washukiwa wa ugaidi kwa kuwatosa ndani ya maji ambao umepingwa vikali nchini Marekani. Kwamba Brown atatumia kura yake kuyakwamisha mageuzi ya chama cha Democratic ni jambo ambalo si la kutilia shaka.

Kitaifa athari za matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Massachussetts zimedhirika wazi huko Marekani. Hata hivyo inasubiriwa kuona ni athari gani zitakazojitokeza katika sera ya nje ya rais Obama. Katika sera ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, rais Obama hawezi kuendelea kuwa na jukumu la kuongoza katika ngazi ya kimataifa.

Bila idhini ya bunge la Marekani, rais Obama hawezi kutoa ahadi za kuaminika katika ngazi ya kimataifa na siasa za ndani ya nchi zitamlazimu kiongozi huyo atumie muda wa ziada na nguvu zaidi. Ni kusubiri kuona ni mada zipi za kimataifa zitakazobakia.

Rais Obama inadhaniwa atapata utulivu haraka kutokana na mshangao alioupata baada ya matokeo ya uchaguzi wa Massachussetts na atatafuta njia nyingine za kuiongoza Marekani vyema licha ya upinzani huu. Sera ya kufanya mabadiliko makubwa ambayo amekuwa akiisisitiza sana, sasa haiwezekani tena.