1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Museveni wa Uganda atoa onyo kali kwa maafisa wake

Emmanuel Lubega 16 Machi 2023

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewaonya viongozi na maafisa katika serikali yake kwamba atawachukulia hatua kali kutokana na mienendo yao ya kuiba pesa za umma ambazo zililengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

https://p.dw.com/p/4OoFU
EAC Staaten Video-Konferenz | Yoweri Museveni
Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

Akilhutubia bunge na taifa alasiri ya leo, Rais Museveni amewakaripia viongozi na maafisa wa ngazi za juu serikalini kwa kuhujumu mipango yake ya kuwakwamua raia kutoka kwenye umasikini sehemu mbalimbali za nchi. Amewaonya kuwa hatawafumbia macho tena na watachukulia hatua za kisheria. 

Agizo la Museveni lazua mshangao Uganda

Raia wa Uganda waliosubiri hotuba hiyo kwa hamu kubwa walimtarajia Rais Museveni kuongea kuhusu masuala ambayo hivi karibu yametawala maisha yao, ufisadi unaowahusisha mawaziri wa ngazi za juu katika serikali yake.

Wengi wameelezea kuvunjika moyo kwamba hakugusia suala la wizi wa mabati yaliyokusudiwa kwa ajili ya watu wa jamii ya Karamoja ambapo mawaziri kadhaa wa ngazi za juu wamehusishwa.

Museveni aadhimisha miaka 37 tangu alipoingia madarakani

Rais Museveni pia amegusia kuhusu mapenzi ya jinsia moja pamoja na suala la ulawiti ambayo yamekuwa mjadala unaotawala kwa sasa kutokana na madai kwamba umezagaa katika jamii.

Kikao maalum cha bunge ambacho kimefanyika leo ni mojawapo na majukwaa ambapo rais huelezea hali ilivyo nchini na kufafanua kuhusu jinsi serikali inavyoyashugulikia masuala kadha wa kadha.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.