1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Museveni akosolewa kuhusu mpango wa usalama kwa wabunge

Lubega Emmanuel29 Juni 2018

Rais Museveni ataka wabunge wapewe walinzi kuwahakikishia usalama, lakini pendekezo hilo limekosolewa na watu mbalimbali wakiwemo wabunge wenyewe

https://p.dw.com/p/30Z2O
Yoweri Museveni Präsident Uganda
Picha: Imago/ITAR-TASS/A. Shcherba

Agizo la Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuwa kila mbunge apewe walinzi kama njia ya kuwakikishia usalama wao limekosolewa na watu mbalimbali wakiwemo wabunge wenyewe. Wana maoni kuwa hilo huenda lisiwe suluhu la kudumu kwa usalama wa nchi ambao umetajwa kuendelea kuzorota siku za hivi karibuni. Kwa mtazamo wao kiongozi huyo angezingatia chanzo cha wabunge na viongozi wengine wa kisiasa kupokea vitisho kwa maisha yao kwani mauaji yas Mnayofanyika huenda yana ujumbe unaolenga utawala wake na wala si watu binafsi.

Hao ni wakereketwa wa haki za wanawake wakianzisha kampeni yao ya kuikosoa serikali ya Uganda kuhusu kuzorota kwa usalama, kielelezo chake kikiwa wimbi la utekaji nyara na mauaji ya kikatili ya watu wa matabaka na umri mbalimbali. Mwezi huu wa Juni, Rais Museveni alihutubia wabunge na taifa kwa jumla mara tatu akitilia mkazo suala la usalama wa wananchi na mali zao. Katika mojawapo ya vikao, rais aliahidi kumpa kila mbunge mlinzi ili kumhakikishia usalama wake. Bunge la Uganda lina wabunge 438.

Hii ina maanisha kuwa idadi kama hiyo au zaidi ya walinzi itahitajika kuwahakikishia usalama wao kila waendako. Lakini baadhi ya wabunge wametoa mtazamo kuwa hii haitondoa hofu na mashaka kwao kwani wale wanaotenda mauaji hawalengi wabunge tu lakini huwaua hata walinzi kama ilivyokuwa kwa maarehemu Ibrahim Abiriga aliyeuawa wiki tatu zilizopita. Wanapendekeza chanzo cha chuki na uhasama kwa viongozi kichunguzwe ili taifa lote lifikie suluhu la kudumu kuhusu usalama.

Bunge la Uganda
Bunge la UgandaPicha: Reuters/J.Akena


Suala la ulinzi wa wabunge limekuwa nyeti hata katika nchi jirani ya Kenya ambapo walinzi na madereva wamewahi kuwasilisha malalamiko yao kuhusu mazingira magumu wanamofanyia kazi ikiwemo kuendesha shughuli binafsi za waheshimiwa kama vile kutumwa sokoni, kuwapeleka watoto shuleni na kadhalika. Wakati huohuo kuna maoni mbalimbali kama kweli wabunge wanahitaji ulinzi na kwa kiwango gani kwani ni wawakilishi wa watu waliowachagua kwa hiari yao. Ni kwa ajili hii ndipo kuna maoni kwamba usalama wa raia wote ushughulikiwe kwa kuwepo na jeshi la polisi ambalo linatosheleza mahitaji pamoja na kuwezeshwa kuendesha kazi zao katika mazingira muafaka.
 

Watetezi wa haki za wanawake nao wamekosoa hatua ya kuangazia tu ulinzi wa wabunge na watu mashuhuri ili hali asli mia 60 ya visa vya uhalifu huhusiana na kuwanyanyasa wanawake. Wanadai kuwepo kwa vitengo maalum vya kushughulikia usalama wao kwa kuzidisha idadi ya askari polisi wanawake. Nchini Uganda asli mia 18 tu ya askari polisi ni wanawake ili hali watu wa jinsi hiyo wanajumuisha zaidi ya asli mia 52 ya idadi ya watu.
 

Kwa mara ya kwanza hapo kesho Jumamosi, ulimwengu utaadhimisha siku ya kimataifa ya ubunge kwa kuangazia taasisi hiyo kuwa mhimili wa demokrasia ili kuboresha maisha ya watu wanaowakilishwa. Swali ni je mbona wabunge wanaendelea kupokea vitisho au kuhisi kwamba maisha yao yamo hatarini kiasi cha kupewa ulinzi maalum.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala

Mhariri: Mohammed Khelef