1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden alalamikia vizingiti vinaavyowekwa na utawala wa Trump

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
29 Desemba 2020

Rais mteule wa Marekani Joe Biden amesema kutokuwepo mawasiliano kati ya maafisa wa usalama na timu yake ya mpito ni hatua inayoweza kudhoofisha hali ya usalama wa Wamarekani. 

https://p.dw.com/p/3nJUl
Wilmington, USA | Rede Joe Biden Videokonferenz Außenpolitik
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Rais mteule wa Marekani Joe Biden amelalamika juu ya vizingiti vinavyowekwa na utawala wa Trump katika kipindi cha mpito. Biden amesema mashirika ya usalama yamehujumiwa chini ya utawala wa Trump na ameeleza kuwa ni kitendo cha kutowajibika kuzuia ripoti kwa utawala ujao. Ameeleza kuwa timu yake inakabiliwa na vizingiti kwenye serikali ya Trump, kuanzia kwenye wizara ya ulinzi hadi kwenye idara za  usimamizi na bajeti.

Soma Zaidi: Joe Biden athibitishwa rasmi kuwa rais ajae wa Marekani

Rais mteule Biden alisema hayo baada ya kukutana na timu yake itakayoshughulikia masuala ya nchi za nje, usalama wa taifa, ulinzi na washauri wake, wakiwemo mawaziri wake wateule wa mambo ya nje, ulinzi, mambo ya ndani pamoja na mshauri wa usalama wa nchi ajae.

Makamu mteule wa rais wa Marekani Kamala Harris
Makamu mteule wa rais wa Marekani Kamala HarrisPicha: C-Span/ZUMA Wire/Zumapress/picture alliance

Amesema kwa sasa hawapati ripoti zote zinazohitajika juu ya maeneo muhimu ya usalama kutoka kwa utawala wa Trump unaokaribia  kuondoka madarakani. Amesisitiza kwamba kikosi  chake  kinahitaji ripoti  zote juu ya mchakato wa bajeti ya wizara ya ulinzi

Mpaka sasa rais Trump bado amekataa kukubali kuwa alishindwa kwenye uchaguzi kwa zaidi ya kura milioni 7, na utawala wake haukuidhinisha mapema ushirikiano rasmi na timu ya mpito ya Biden hadi Novemba 23, wiki baada ya uchaguzi.

Biden amesisitiza kuwa changamoto kuu itakayowakabili yeye na makamu wake wa rais Kamala Harris ni kuzijenga upya idara za mambo ya nje na ile ya usalama wa taifa mara watakapoanza kazi mnamo Januari 20 mwakani.

Vyanzo:/AP/https://p.dw.com/p/3nIk3