1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Marekani Donald Trump ahanikiza Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Januari 2017

Sera za rais wa Marekani Donald Trump pamoja na makadirio ya serikali kuu mpya nchini Ujerumani baada ya chama cha kiliberali FDP kumuunga mkono Frank Walter Steinmeier awe rais wa shirikisho ndio mada kuu magazetini

https://p.dw.com/p/2WIZ0
USA steigen aus Transpazifik-Handelsabkommen aus
Picha: Reuters/K. Lamarque

Tunaanzia Marekani ambako rais mpya Donald Trump anaanza kutekeleza kile alichokipigia upatu katika kampeni za uchaguzi. Kwanza dhidi ya vyombo vya habari anavyodai vinaeneza uwongo. Gazeti la "Pasauer Neue Presse" linaandika: "Kifanywacho na Trump si mabishano ya kawaida ya kidemokrasi, ni mapambano ya moja kwa moja dhidi ya misingi ya demokrasia. Mtu anaewaita wawakilishi wa vyombo vya habari kuwa ni "waongo," kwa sababu ya uwezo  wao wa kupima , yeye mwenyewe lakini akijipa haki ya kutumia kile anachokiita " ukweli mbadala", mtu kama huyo ni mwenye kiburi  na anapokuwa kiongozi wa nchi, basi ni hatari zaidi kwasababu anaweza kufuata mtindo wa mtawala wa kiimla anaelinganisha kila lawama dhidi yake kuwa ni sawa na kumtusi. Wamarekani bado hawajakiona kilichomtoa kanga manyoya, kwasababu kauli mbiu "America first" tafsiri yake si nyengine isipokuwa "Trump first."

Makubaliano ya biashara TPP yamefutwa

"America first" anaitumia pia rais mpya wa Marekani Donald Trump ili kubatilisha makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa na mtangulizi wake Barack Obama. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika: "Donald Trump anatisha kweli kweli. Marekani inajitoa katika mkataba wa biashara wa nchi zinazopakana na bahari ya Pacifik-TPP. Makubaliano ya biashara huru pamoja na nchi za Asia yana maana gani, ikiwa kwanza inakuja Marekani na baadae hakuna chochote kinachofuata-kwa mujibu wa upeo wa macho wa rais wa Marekani. Donald Trump anapendelea zaidi makubaliano ya nchi kwa nchi ili apate kumdhibiti ipasavyo adui. Na anataka kuyaadhibu makampuni yatakayosubutu kuendesha shughuli zao nje ya upeo wa macho yake. Wakati huo huo anataka kupunguza kodi za mapato kwa makampuni kwa kati ya asili mia 15 hadi 20, ili lisitokee kampuni lolote litakalohamishia shughuli zake ng'ambo.

Pengine nchi za Ulaya zinaweza pia kurahisisha mambo. Makampuni makubwa makubwa ya Marekani mfano wa Apple, Microsoft, Amazon au Facebook yanaendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa barani Ulaya, lakini kodi zinazolipwa na makampuni hayo ni kidogo sana. Kwa mujibu wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya, mwaka 2014  Apple ililipa kodi ya mapato ya asili mia 0.005. Mpaka Trump angekiri kuwa ni haba mno, kwa hivyo Umoja wa Ulaya unabidi uzinduke."

Ishara serikali kuu inayokuja itakuwa ya aina gani

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na makadirio, serikali ya aina gani itaundwa baada ya uchaguzi mkuu wa september 24 mwaka huu nchini Ujerumani. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linachambua uamuzi wa chama cha kiliberali cha FDP kumuunga mkono Frank-Walter Steinmeier achaguliwe kuwa rais wa shirikisho, mhula wa rais wa sasa Joachim Gauck utakapomalizika mwezi unaokuja. "Imeshadhihirika kwa hivyo, kama inavyokuwa katika chaguzi kadhaa za rais, na mara hii pia zoezi la kumchagua rais wa shirikisho litaashiria pia muundo wa serikali utafuata mkondo gani. Uwezekano wa kuendelezwa serikali ya muungano wa vyama vikuu upo. Na pindi SPD, walinzi wa mazingira die Grüne na waliberali FDP watajikingia nukta zaidi, basi na wao pia wanaweza kuunda serikali ya muungano wa vyama vitatu.

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Gakuba Daniel