1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Morsi apuuzilia mbali onyo la jeshi la Misri

Admin.WagnerD2 Julai 2013

Rais wa Misri Mohammed Morsi ameishutumu hatua ya jeshi la nchi hiyo ya kutoa muda wa saa 48 kwa Rais huyo kutimiza matakwa ya raia katika mzozo wa kisiasa nchini humo au litajiingiza kati.

https://p.dw.com/p/1907G
Picha: Reuters

Rais Morsi leo amesema kuwa hakushauriwa na jeshi kabla ya kuafikia uamuzi huo wa kuwekwa kwa makataa na kwamba ataendelea na mipango yake ya kuafikia maridhiano ya kitaifa licha ya kile alichokitaja kutolewa kwa taarifa za kuligawanya taifa.

Lakini kiongozi huyo wa kiislamu anaonekana kuzidi kutengwa huku upande wa upinzani wa kiliberali ukikataa kuzungumza naye na jeshi linaloungwa mkono na mamilioni ya waandamanaji wanaomtaka ang'atuke madarakani ikimpa hadi kesho kukubali kugawana madaraka.

Masaibu ya Morsi yazidi

Shinikizo dhidi ya Rais huyo wa Misri linazidi huku waziri wake wa mambo ya nje Mohammed Kamel Amr akiwa miongoni mwa mawaziri ambao wamejiuzulu tangu maandamano hayo kuanza Jumapili wakiwemo mawaziri wa utalii,mazingira,uwekezaji na sheria .

Waandamanaji wanaomtaka Rais Morsi kung'atuka madarakani waandamana Cairo
Waandamanaji wanaomtaka Rais Morsi kung'atuka madarakani waandamana CairoPicha: Reuters

Na mahakama ya juu ya rufaa leo imebatilisha uamuzi wa mahakama ya kumuondoa mwendesha mkuu wa mashitaka Abdel Meguid Mahmud aliyefutwa kazi mwezi Novemba mwaka jana na Morsi na kuzua uhasama kati ya idara ya mahakama na Rais huyo.

Magazeti nchini humo yameangazia pakubwa agizo la jeshi huku mengi yao yakiwa na kichwa cha saa '48 za mwisho kwa utawala wa udugu wa kiislamu' na magazeti mengine yakiandika 'Misri yalisubiri jeshi'.

Mzozo huo umelitumbukiza taifa hilo la kiarabu katika hali ya kukata tamaa huku kukiwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi miaka miwili baada ya kuondolewa madarakani kwa Hosni Mubarak na kuzua wasiwasi kwa Marekani,Ulaya na nchi jirani ya Israel.

Waandamanaji wamekesha katika uwanja wa Tahrir mjini Cariro na viongozi wao wameitisha maandamano mengine leo jioni kujaribu kumng'oa madarakani rais.Mmoja wa waandamanaji hao amesema hata hizo saa 48 ni muda mrefu

Hata hivyo wafuasi wa Morsi ambao pia wameandamana kutetea uhalali wake madarakani wamesema jaribio la kumuondoa madarakani rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ni sawa na mapinduzi ya serikali

Mkuu wa jeshi la Misri Abdel-Fattah al-Sissi
Mkuu wa jeshi la Misri Abdel-Fattah al-SissiPicha: picture-alliance/dpa

Jeshi limekanusha kufanya jaribio la mapinduzi na kusema taarifa ya mkuu wa majeshi Abdel Fattah al Sisi ilipaswa kuzishinikiza pande zote mbili za kisiasa kupata suluhisho la haraka kwa mzozo unaoendelea. Morsi ndiye rais wa kwanza Misri kuchaguliwa katika uchaguzi huru na wa haki.

Morsi ambaye ni kiongozi wa muda mrefu wa udugu wa kiislamu wenye ushawishi mkubwa nchini humo aliingia madarakani mwaka mmoja uliopita kufuatia wimbi la maasi mwaka 2011 ambayo yalimaliza uongozi wa kiimla wa miongo mitatu wa Hosni Mubarak.

Rais huyo wa Misri pia amezungumza na Rais wa Marekani Barrack Obama kwa njia ya simu hapo jana kuhusiana na yanayojiri nchini humo na afisi ya Rais wa Marekani imesema Morsi amehimizwa kushughulikia matakwa ya wanaoandamana kwani mzozo huo unaweza tu kusuluhishwa kupitia mchakato wa kisiasa.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman