1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Magufuli achukua fomu za kuwania urais tena

17 Juni 2020

Rais wa Tanzania John Magufuli amechukuwa fomu za uteuzi kutafuta ridhaa ya chama chake cha CCM kuwania muhula wa pili katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/3duhS
Tansania Bashiru Ali (L) und Präsident John Pombe Magufuli
Picha: State House Tanzania

Rais Magufuli amekabidhiwa fomu hizo mapema leo kwenye makao makuu ya chama mjini Dodoma, na Katibu Mkuu wa CCM Bashiru Ally.

Nderemo na vifijo vilitawala katika makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM mjini Dodoma wakati Rais John Magufuli alipowasili kwa ajili ya kuchukua fomu ya kukiomba ridhaa chama chake akiwakilishe katika kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Punde tu baada ya kukabidhiwa fomu hiyo na katibu mkuu wa chama chake Dokta Bashiru Ally, Rais magufuli aliwashukuru wanachama na wafuasi wa CCM waliohudhuria katika ofisi hizo kwa lengo la kushuhudia zoezi hilo ambalo linakwenda kwa mujibu wa katiba ya chama chake.

Hakuna mwengine aliyejitokeza kuchukua fomu mbali na Pombe Magufuli

Magufuli amesema amekuwa akipigiwa simu na makada wa chama hicho kikongwe nchini na kumuahidi kumdhamini, hivyo ataanzia mkoa wa Dodoma katika kutafuta wadhamini wasiopungua mia mbili hamsini ili awahi kurejesha fomu hiyo mapema iwezekanavyo.

Chama Cha Mapinduzi, CCM kilifungua milango yake ya watangaza nia kwa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2020, lakini hadi sasa kwa upande wa Tanzania Bara hajajitokeza kada mwingine wa chama hicho kuchukua fomu mbali na Rais Magufuli.

Je katika awamu hii huenda Rais Magufuli asikabiliane na upinzani wa kutetea awamu yake ya pili ya uongozi na ya mwisho kikatiba?

Kama Rais Magufuli atapitishwa na chama chake kukiwakilisha katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atachuana na wagombea wa vyama vya siasa vya upinzani kwa ajili ya kutetea kiti chake cha urais kwa awamu ya pili alichokalia tangu Novemba 5, 2015.