Rais Kiir na Machar wakubaliana kuhusu usalama | Matukio ya Afrika | DW | 06.07.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Kiir na Machar wakubaliana kuhusu usalama

Shirika la habari la serikali ya Sudan, SUNA, limeripoti Alhamisi jioni (05.07.2018) kwamba serikali ya Sudan Kusini na waasi wameafikiana juu ya utaratibu wa usalama wakati wa mazungumzo mjini Khartoum.

Mazungumzo hayo yamekuwa yakisimamiwa na Sudan, taifa ambalo Sudan Kusini ilijitenga nalo na kujitangazia uhuru wake 2011 baada ya miongo kadhaa ya umwagaji damu. Sudan Kusini yenyewe ilitumbukia katika vita miaka miwili baadaye wakati mzozo wa kisiasa kati ya rais Salva Kiir na makamu wake wakati huo, Riek Machar, ulipolipuka na kugeuka kuwa mapambano ya kijeshi.

Mwezi uliopita, rais Kiir alisaini muongozo wa mkataba na kiongozi wa waasi Machar mjini Khartoum ulioruhusu usitishwaji mapigano, na kufungua mlango kwa mazungumzo kuelekea mkataba kamili.

Lakini waasi kwa haraka walivikataa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo na pande zote mbili zimenyosheana kidole cha lawama kwa kutoyaheshimu mapatano ya kusitisha mapigano, wakilaumiana kwa mashambulizi ambayo yamesababisha vifo vya raia 18.

Shirika la habari la SUNA Alhamisi jioni lilimnukuu msemaji wa jeshi la Sudan, Brigedia Jenerali Ahmed Khalifa al-Shami, akisema pande mbili zinazohasimiana za Sudan Kusini zilikuwa zimekamilisha mkataba kuhusu masuala ya usalama na kuandaa rasimu itakayosainiwa mbele ya rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, katika tarehe ambayo haikutajwa.

Shami alisema mkataba huo umezingatia masuala manne makuu - kuondosha vituo vya kuwashikilia watu vilivyosimikwa na majeshi, muda wa kuliungnisha na kulifanyia mageuzi jeshi la Sudan Kusini, kuanzisha kamati ya pamoja kuhusu masuala ya usalama, na kuamua juu ya maeneo ambako wanajeshi wanatakiwa kukaa.

Mapigano nchini Sudan Kusini yamesababisha takriban asilimia 25 ya wakazi kuyakimbia makazi yao, kuvuruga uzalishaji wa mafuta na kuusambaratisha uchumi wa taifa hilo ambao tayari ulikuwa katika hali taabani.

Mwandishi: Josephat Charo/rtre/

Mhariri: Mohammed Khelef