1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kibaki kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika Addis Ababa

Josephat Charo31 Januari 2008

Mkutano wa Umoja wa Afrika kujadili mzozo wa Darfur, Somalia, Kenya na ujenzi wa viwanda

https://p.dw.com/p/D05h
Rais Mwai Kibaki (kulia) na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika rais wa Ghana John Kufuor walipokuwa mjini NairobiPicha: picture-alliance/dpa

Rais Mwai Kibaki wa Kenya anaondoka leo mjini Nairobi kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.

Kiongozi huyo anatarajiwa kuondoka mjini humo mwendo wa saa moja unusu asubuhi ya leo licha ya mzozo wa kisiasa unaoendelea kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.

Atakapokuwa mjini Addis Ababa rais Kibaki atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa shirika la maendeleo la kanda ya Afrika Mashariki, IGAD.

Chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement, ODM, kilimtuma katibu mkuu wake, Profesa Anyang Nyong´o mjini Addis Ababa mapema juma hili kuushinikiza Umoja wa Afrika usimruhusu rais Kibaki kuhudhuria mkutano huo.

Chama hicho kinadai kumualika rais Kibaki katika mkutano wa mjini Addis Ababa ni kutambua rasmi kuchaguliwa kwake tena na kuzihujumu juhudi za upatanisho zinazoongozwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan.

Mazungumzo kati ya pande zinazozana yanaingia siku yake ya pili hii leo huku shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu, Amnesty International, likiitolea mwito serikali ya Kenya iwalinde wanaharakati wa haki za binadamu, ambao baadhi yao wamepokea vitisho vya kuuwawa kwa kulaani udanganyifu uliotokea katika uchaguzi uliopita.

Maafisa tisa, wakiwemo wanaume sita na wanawake watatu wamepokea ujumbe unaowashutumu kwa kuyasaliti makabila yao.

Zaidi ya viongozi 40 wa nchi za Afrika wanahudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.

Mkutano wa siku tatu wa umoja huo wenye wanachama 53 unaanza leo na unatarajiwa kujadili juhudi za amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan, machafuko yanayoendelea nchini Somalia na mada rasmi ya ujenzi wa viwanda.

Swala lengine litakalojadiliwa katika mkutano huo ni vipi kuishughulikia Kenya.

Shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka limeutolea mwito mkutano wa mjini Addis Ababa kuilaani na kuiwekea vikwazo Eritrea kwa kuwatesa wafungwa.

Shirika hilo limetoa mwito huo baada ya kuchapisha ripoti yake ikiilaumu serikali ya Eritrea kwa kutumia vitendo vya ukatili dhidi ya watu inaowaona kuwa hatari.

Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limemtaka katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amshinikize hadharani rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, akubali waranti wa kukamatwa kwa raia wawili wa Sudan wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur.

Ban Ki Moon atakutana na rais Bashir kandoni mwa mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa akiwa na matumaini ya kuondoa vikwazo dhidi ya jeshi la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika la kulinda amani Darfur.