Rais Kenyatta na viongozi wa Kenya wamuomboleza Mkapa | Matukio ya Afrika | DW | 24.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Kenyatta na viongozi wa Kenya wamuomboleza Mkapa

Rais Uhuru Kenyatta amewaongoza wakenya kutuma risala za rambirambi kwa familia ya rais wa awamu ya tatu wa Tanzania Benjamin William Mkapa. Kenyatta amewatakia Watanzania wote faraja.

Kwenye ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amemtaja mwendazake Benjamin Mkapa kuwa kiongozi aliyejitolea kuhakikisha umoja na utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akizingatia Amani na maendeleo kwenye kanda hii. Rais Kenyatta ameitakia familia ya Mkapa na Watanzania wote faraja wakati huu mgumu wa msiba.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika aliye pia kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga aidha amejiunga na Wakenya wengine kumuomboleza rais mstaafu wa awamu ya tatu nchini Tanzania Benjamin Mkapa.

Mchango wa Mkapa kwa amani ya Kenya

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Raila amemtaja Mkapa kuwa rafiki wa karibu wa taifa la Kenya. Raila aliongeza kusema kuwa marehemu alikuwa Mwanaafrika halisi aliyeamini muungano wa bara hili.

Taarifa hiyo ilisema, "nchini Kenya, tumehifadhi kumbukukumbu nzuri za marehemu. Tunakumbuka juhudi zake pamoja na za aliyekuwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Daktari Koffi Annan na Graca Machel ambazo zilichagia kuzima ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya kati ya mwaka 2007-2008.

Benjamin Mkapa alikuwa miongoni mwa wapatanishi walioshughulikia amani ya Kenya baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2008.

Benjamin Mkapa alikuwa miongoni mwa wapatanishi walioshughulikia amani ya Kenya baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2008.

Rais Mstaafu Mwai Kibaki amemtaja Mkapa kuwa mmoja wa wana wakuu wa Afrika. Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Kibaki amesema kuwa kwa wakati mmoja Mkapa aliongoza mazungumzo ya Amani katika mataifa ya Kenya, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Zimbabwwe Sudan Kusini na Burundi.

Mkapa alichangia pakubwa Amani nchini Kenya, taifa lilipotumbukia kwenye vita baada ya uchaguzi mkuu uliokumbukwa na utata mwaka 2007 Kibaki alipokuwa rais. Zaidi ya watu elfu moja waliuawa huku wengine nusu milioni wakipoteza makazi kwenye ghasia hizo.

Baada ya kufualu kuliunganisha taifa la kenya kwenye mzozo, mwaka 2008 Mkapa aliandika kitabu kilichoelezea jinsi alivyowazuia William Ruto ambaye ni makamu wa rais nchini Kenya na Martha Karua aliyekuwa waziri wa masuala ya kikatiba kwenye mkutano, ambao uliwaleta pamoja rais Mwai Kibaki na kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga kwenye meza duara ya mazungumzo. Mazungumzo hayo yalichangia kubuniwa kwa serikali ya pamoja kati ya rais Kibaki na Raila Odinga aliyepewa wadhfa wa kuwa waziri Mkuu.

Rais Benjamin Mkapa, aliongoza Tanzania kati ya mwaka 1995 hadi 2005 alipompisha Jakaya Mrisho Kikwete.