1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kagame wa Rwanda atembelea Ujerumani

Dreyer, Maja24 Aprili 2008

Leo usiku, rais wa Rwanda, Paul Kagame, alimaliza ziara yake nchini Ujerumani. Mara kadhaa tayari, raisi huyu aliitembelea Ujerumani kukutana na viongozi wa serikali na sekta ya uchumi.

https://p.dw.com/p/DoAV
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akimkaribisha rais Paul Kagame wa RwandaPicha: picture-alliance/ dpa

Kwa muda wa siku mbili, rais Paul Kagame aliitembelea Ujerumani akikutana na viongozi mbali mbali wa serikali na uchumi. Ujerumani ni mshirika muhimu wa kibiashara, na katika mahojiano, raisi huyu aliyofanya na DW-TV, alisema kwamba Rwanda ina nafasi nzuri kujiendeleza akitaja kwamba Rwanda inataka kuchukua mfano wa Singapur barani Asia.


Rais Kagame alisema: “Bila shaka kuna mifano mingi mizuri duniani ambayo inaweza kutoa mafunzo na ninadhani Singapur imefanya vizuri kwa kutega katika wananchi wake na kuwachukua rais kama rasili mali muhimu zaidi ambayo itaweza kuleta maendeleo na kufika kiwango cha nchi za dunia ya kwanza. Rwanda inaweza kufanya hivyo hivyo, inategemea tu kuchukua njia inayoifaa nchi yetu. Lakini ninaamini kwamba kuna nafasi nzuri tutaweza kujiendeleza, inabidi tu tuchape kazi na kujipange vizuri.”


Suala ambalo Wajerumani wengi wanajiuliza wakifikiria Rwanda ni vipi nchi hii iliweza kuendelea baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.


Akiulizwa kuhusu vipi maridhiano yanavyoendelea alikuwa na haya ya kusema: “Maridhiano yaliendelea vizuri kuliko tulivyotarajia, yaani yalitimiza matumaini yetu kupita kiasi. Ukiangalia kwamba miaka 14 baada ya mauaji ya kimbari, watu wa Rwanda wanafanya kazi kwa pamoja na wanaishi pamoja kwa amani. Kimsingi, usalama nchini Rwanda uko imara kuliko kwengineko katika eneo letu.”


Kuhusu kazi ya Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita nchini Rwanda, ICTR, rais Kagame hakuridhika. Hapo alisema ukilinganisha muda na gharama mahakama hiyo iliotumia na idadi za kesi zilizoendeshwa, hakuna usawa.


Misaada ya maendeleo yalitajwa pia katika mahojiano haya, baada ya nchi za Magharibi zilipoamua kutoa fedha nyingi zaidi kuleta maendeleo barani Afrika. Rais Kagame alikiri kuwa Afrika imeshapokea kiwango kikubwa cha malipo ya misaada ya miaka iliyopita, lakini hakuna mengi yaliyotokana na haya. Kama sababu, rais huyu ameleza hivi: “Misaada hiyo ya kigeni haikulenga vizuri, haikutumika katika eneo mwafaka  na kwa namna ambayo ingewasaidia Waafrika kuweka msingi wa kujenga maendeleo.”


Kagame anaendelea kusema kwamba kwa sababu hiyo, msaada ulitolewa haukusaidia nchi za Afrika wala nchi za Magharibi. Kwa hivyo, inabidi sera za maendeleo za nchi wafadhili ziangaliwe upya kabisa. Na kwa wakati huo huo, nchi za Kiafrika pia zinabidi kufikiria upya mbinu zao, alisisitiza rais Kagame: “Ili nchi hizo zisitegemee msaada bali zizipe kipaumbele juhudi za kutumia uwezo wao maalum. Kuna utajiri mkubwa barani Afrika lakini Waafrika hawakuweza kutumia utajiri huu vizuri kwa ajili ya maendelo yao. Kwa hivyo basi, jukumu la nchi za Kiafrika ni kubwa kuliko la nchi za Magharibi.”


Utawala bora unasemekana kuwa ni njia moja ya kuleta mabadiliko na maendeleo na rais Paul Kagame wa Rwanda katika mahojiano haya na Deutsche Welle alisema kwamba lazima kuwepo kwa mabadiliko katika maadili ili kuwepo maendeleo.


Kuhusu suala la Zimbabwe na mzozo wa kisaisa nchini humo, Kagame alikumbusha juu ya umuhimu wa uchaguzi: “Ndiyo sababu, uchaguzi ulifanyika nchini Zimbabwe, ili watu waweze kutoa maoni yao na kuchagua wenyewe, lakini sasa inaonekana kama utaratibu huu ulikuwa unayumba na kitu kisicho halali kimetokea. Basi ikiwa Wazimbabwe wanashindwa kutatua hali hii wenyewe, nchi jirani, nchi za Kiafrika na jumuiya ya kimataifa itawasaidia kutafuta suluhisho.”