Rais Köhler atembelea nchi za Ulaya Mashariki Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Köhler atembelea nchi za Ulaya Mashariki Kusini

Rumania, Bulgaria na Bosnia – hizo ndizo nchi rais Horst Köhler wa Ujerumani anazitembelea katika ziara yake ya Ulaya Mashariki Kusini wiki hii. Kabla ya kulitembelea jeshi la Ujerumani liloko Bosnia, Köhler ameanza ziara yake katika nchi hizo nyingine Rumania na Bulgaria nchi ambazo zimejiunga na Umoja wa Ulaya mwanzoni mwa mwaka huu.

Rais Köhler na mwenzake rais Parvanov wa Bulgaria

Rais Köhler na mwenzake rais Parvanov wa Bulgaria

Ni ziara ya kuwakaribisha katika Umoja wa Ulaya nchi hizo mbili za Ulaya Mashariki ya Kusini, Rumania na Bulgaria ambazo kujiunga kwao kulikuwa jambao lisilokubaliwa na wote. Rais Horst Köhler lakini ameweza kuigusu mioyo ya wananchi wa mataifa haya mawili pale mwanzoni mwa ziara yake pale aliposema kuwa anafurahi kuwa Rumania na Bulgaria zimerudi katika familia ya nchi za Ulaya zikiwa sawa na nchi nyingine wanachama wa Umoja huo.

Köhler hasa alisifu juhudi za nchi hizo mbili katika kuuunga mkono mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya uliokubaliwa hivi karibuni kwenye mkutano wa kilele wa Umoja huo mjini Brussels. Vilevile alizipongeza serikali za nchi hizo kwa maendeleo mazuri ya kidemokrasia baada ya kutokea mageuzi ya kisiasa miaka 18 iliyopita pamoja na kusisitza ushirikiano wao wa kibiashara na Ujerumani ambao ni muhimu sana kwa Rumania na Bulgaria.

Hata hivyo, Köhler pia alitoa mwito kwa serikali zote mbili kutolegeza jitihada za kutekeleza mageuzi. Mjini Bukarest, huko Rumania, alitaja matatizo katika mfumo wa sheria. Mageuzi yaendelee kutekelezwa alisema Köhler na akaongeza: “Muhimu hasa ni juhudi za kuwa na mahakama huru na mfumo wa sheria unaofanya kazi vizuri pamoja na vita dhidi ya rushwa kwenye ngazi zote.”

Rais wa Rumania, Bw. Traian Besescu, akiulizwa kujibu ukosoaji huu amemwunga mkono rais Köhler wa Ujerumani: “Rumania kwa kupitia idara zake inapaswa kuchukua hatua dhidi ya rushwa kwa thabiti zaidi, kwa nguvu zaidi na kwa na moja.”

Hali ya rushwa huko Rumania na Bulgaria haina mithili barani Ulaya kote. Chau-chau inatakiwa katika kila sehemu ya maisha kutokana na mishahara ya chini hasa kwenye upande wa wafanyikazi wa serikali.

Nchini Bulgaria rais Köhler hakuwa na wasiwasi kuzungumzia wazi matatizo yaliyopo, kama kawaida yake. Bw Köhler ametaja masuala ya usalama wa sheria, makundi ya kihalifu na rushwa kwenye ngazi ya juu. Huko pia, mwenzake rais wa Bulgaria alimwahidi Köhler kuendelea na mageuzi yake.

Lakini ziara ya rais Köhler si juu ya siasa tu, bali pia Köhler alitembelea mji wa Hermannstadt huko Bulgaria ambao mwaka huu unachukua nafasi ya mji mkuu wa mambo ya utamaduni katika Umoja wa Ulaya. Kwake rais wa Ujerumani, mji huu una umuhimu maalum, kwani ni asili ya familia ya mama wake. Ndiyo sababu alifurahi sana kufika katika mji huu ambao umejengwa na Wajerumani zaidi ya miaka 800 iliyopita na ambapo bado wanaishi watu wengi wenye asili ya Kijerumani.

 • Tarehe 04.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHBe
 • Tarehe 04.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHBe
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com