Rais Köhler akataa kutoa msamaha kwa gaidi Christian Klar | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Köhler akataa kutoa msamaha kwa gaidi Christian Klar

Rais Horst Köhler wa Ujerumani amekataa kutoa msamaha kwa aliekuwa gaidi wa kundi la RAF –jeshi jekundu, Christian Klar anaetumikia kifungo cha maisha kwa kosa la mauaji.

Rais Köhler kushoto,gaidi C.Klar kulia

Rais Köhler kushoto,gaidi C.Klar kulia

Taarifa kutoka ofisi ya rais imesema leo alasiri kuwa bwana Köhler pia amekataa kutoa msamaha kwa gaidi mwengine wa kundi hilo bibi Birgit Hogefeld.

Rais wa Ujerumani bwana Köhler alikutana na gaidi Christian Klar ijumaa iliyopita na kueleza baadae kwamba angetafakari ombi la gaidi huyo juu ya kupewa msamaha.

Kauli hiyo ilisababisha malalamiko makubwa miongoi mwa wanasiasa hasa wa vyama vya CDU na CDU vilivyomo katika serikali ya mseto.

Wanasiasa hao wanapinga kuachiwa mapema kwa gaidi huyo hasa kwa kuwa yeye na magaidi wengine wa kundi la RAF wanakataa hadi leo kutoa habari za undani juu ya mauaji waliyofanya.

Baadhi ya wanasiasa wa vyama hivyo walifikia hatua ya kutishia kumnyima kura rais Köhler itakapofika siku ya kurefusha muhula wake, ikiwa angetoa msamaha kwa gaidi Christian Klar aliehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha mnamo mwaka 1982 kwa makosa ya mauaji.

Mbungea mmoja wa chama cha CSU Andreas Scheuer alisema hapo awali kuwa ikiwa rais Köhler atamsamehe gaidi huyo,atalazimika kufikiria iwapo atampa kura yake ili aweze kuendeleaa na muhula wa pili wa urais.

Mbunge mwingine wa chama cha kijani pia alisema haiwezekani kutoa msamaha kwa mwuuaji wa watu wengi

Mashinikizo hayo yumkini yamemfanya rais Horst Köhler apitishe uamuzi wa kukataa kutoa msamaha kwa Christian Klar.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais imeeleza kuwa bwana Köhler alifanya mazungumzo kadha pia na ndugu wa watu waliouawa na magaidi wa RAF.

Juu ya uamuzi wa rais Köhler kukataa kutoa msamaha kwa gaidi Christian Klar waziri mkuu wa jimbo la Hesse Roland Koch amesema kuwa anakubaliana na hatua hiyo. Waziri mkuu huyo amesema kuwa uamuzi wa rais ni sawa.

Gaidi huyo alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kumwuua mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Sigfried Buback mnamo mwaka 1977.

Pia alihukumiwa kwa kumteka nyara na kumwuua mkuu wa idara ya utumishi Hans Martin Schleyer mnamo mwaka huo huo.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com