Rais Joachim Gauck akamilisha ziara Tanzania | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Joachim Gauck akamilisha ziara Tanzania

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck amekamilisha ziara yake ya siku tano nchini Tanzania kwa kuzindua kituo cha kupambana na ujangili, kinachofadhiliwa na Taasisi ya Hifadhi ya wanyama ya Frankfurt, nchini Ujerumani.

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani amehutubia kwenye ukumbi wa bunge la Afrika ya Mashariki, ambapo amezungumza na wawakilishi wa asasi za kijamii, na hasa mahsusi vijana wa Jumuiya hiyo, ambao wamepewa dhima ya kuufikisha ujumbe wa ushirikiano na maendeleo kwenye jamii zao.

Hotuba ya takribani dakika ishirini ya Rais Gauck imegusia mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama kigezo cha ushirikiano wa kikanda barani Afrika, akisema kwamba ni vijana ndio ambao sasa wanachukuwa jukumu la mageuzi makubwa yanayoweza kuifikisha jumuiya hiyo na bara zima la Afrika kwenye enzi za maendeleo, kujitegemea na kutatua matatizo yake yenyewe.

Vijana wa Afrika wabebaji ndoto ya Afrika

"Ninaamini ni jambo la maana sana kwamba Umoja wa Afrika na hasa vijana kwenye mataifa haya matano wamejitolea kwa ajili ya jamii yao. Kizazi hiki ndicho ambacho kitazifanya ndoto za Afrika kuwa kweli," alisema rais Gauck.

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete pamoja na mkewe Daniela Schadt

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete pamoja na mkewe Daniela Schadt

"Kunahitajika muda kujenga taasisi imara kama Jumuiya ya Afrika Mashariki na hilo linawahitajia vijana kusema tunajaribu kutumia njia mpya, hata kama kuna vigingi vya hapa na pale, tutajaribu tu tusonge mbele," alisema Rais huyo wa Ujerumani.

Vijana aliowazungumzia Rais Gauck ni wale walioteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki chini ya kitengo cha Mabalozi Vijana, wakiwa ni wahitimu na wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka nchi zote wanachama wa huo. Mradi wa mabalozi vijana uko chini ya sekreterieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Peace kutoka Rwanda ni mmoja wa vijana hao ambaye amehudhuria kwenye mkutano huu na Rais Gauck.

Kwetu tunaamini kwenye Jumuiya ya Afrika ya mashariki kama nchi moja na ndio maana tunafanya kila tuwezalo na hotuba hii ya Rais Gauck inatupa matumaini kwamba tunapaswa kuangalia kwenye yaliyo mazuri na kujielekeza yaliyo bora kwa jumuiya yetu.

Gauck azuru bunge la Afrika Mashariki

Mapema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dokta Richard Sezibera, alimueleza Rais Gauck kwamba Ujerumani, ambayo ilifadhili ujenzi wa Bunge la Afrika ya Mashariki ambamo hotuba hiyo imetolewa imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa jumuiya inafanikiwa.

Rais wa Ujerumani Joachim akiwasalimu raia wa Tanzania

Rais wa Ujerumani Joachim akiwasalimu raia wa Tanzania

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Dan Kidega kutoka Uganda, ambaye mwenyewe anatokea kwenye kundi la wabunge vijana nchini kwake, amesema kwamba vijana wa Afrika mashariki wanaweza kuifikisha mbali jumuiya hiyo ikiwa tu watakubali kutokuvunjwa moyo na mawazo na vitendo vinavyowarejesha nyuma miongoni mwa wanajumuiya. Zaidi ya asilimia 50 ya wakaazi milioni 145 wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ni vijana.

Asubuhi ya jana (05.02.2014) Rais Gauck na ujumbe wake walitembelea Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Afrika jijini Arusha ambako alikutana na Rais wa mahakama hiyo, Jaji Augustino Ramadhani na baadaye jioni atakamilisha ziara yake nchini Tanzania kwa kuelekea Seranero, kando kidogo ya mji wa Arusha kuzindua kituo cha kupambana na ujangili, kinachofadhiliwa na Taasisi ya Hifadhi ya wanyama ya Frankfurt, nchini Ujerumani. Asubuhi ya Ijumma,Rais na ujumbe wake watasafiri kurejea Ujerumani.

Mwandishi: Mohammed Khelef

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com