Rais Hosni Mubarak wa Misr ziarani Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Hosni Mubarak wa Misr ziarani Marekani

Rais Hosni Mubarak wa Misr anatarajiwa kukutana leo na maafisa muhimu wa serikali ya Marekani kabla ya kukutana na rais Barack Obama kesho.

default

Rais wa Misr Hosni Mubarak akipunga mkono kwa wajumbe wa bunge la Misr baada ya kuapishwa kuwa rais October 5, 1999.

Rais Hosni Mubarak wa Misri anatarajiwa kukutana leo, Jumatatu, na maafisa muhimu wa serikali ya Marekani , ikiwa ni pamoja na waziri wa mambo ya kigeni, Hillary Clinton, kabla ya kufanya ziara yake ya kwanza katika Ikulu ya Marekani katika muda wa miaka mitano.

Maafisa wa Misri wamesema kuwa Mubarak pia atakutana kwa mazungumzo na mshauri wa taifa wa usalama James, Jones, na mkurugenzi wa ujasusi wa taifa, Dennis Blair, pamoja na kuwa na mkutano wa faragha na wawakilishi kutoka makundi manane ya Wayahudi nchini Marekani.

Miongoni mwa makundi hayo ya Wayahudi ni pamoja na kamati ya masuala ya kijamii kati ya Marekani na Israel, kundi linaloongoza lenye ushawishi nchini Marekani linalopendelea Israel na umoja dhidi ya kuchafua jina la Wayahudi.

Kiongozi huyo wa Misri anatarajiwa kuzuru Ikulu ya Marekani mapema kesho asubuhi katika ziara yake ya kwanza katika ofisi hiyo ya rais kwa mazungumzo na rais Barack Obama. Mkutano huo utakuwa wa tatu katika muda wa miezi kadha, wakati Obama akisisitiza mapema kuwa katika utawala wake atalipa kipaumbele suala la kukwama kwa hatua za mazungumzo ya amani katika mashariki ya kati.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times , kiongozi huyo wa Misr anatarajiwa kuiambia serikali ya Obama kuwa mataifa ya Kiarabu yanataka amani, lakini hayako tayari kukubaliana na wito wa Obama kufikia maridhiano kwa nia njema na Israel hadi pale Israel itakapochukua hatua muhimu kama vile kusitisha kabisa ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika eneo la ukingo wa magharibi.

Tunapaswa kufanya kila linalowezekana kuzileta pamoja pande hizi mbili. Tunapaswa kutafuta suluhisho, tunapaswa kusitisha mzunguko huu unaojirudia. Pande hizi zinapaswa kukaa pamoja na kubadilishana mawazo kwa msaada wa Misr na nchi nyingine. Hakuna njia nyingine.

Mazungumzo ya Mubarak na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya rais Obama pia yanatarajiwa kulenga katika suala la Sudan pamoja na mpango wa kinyuklia wa Iran, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya kigeni wa Misri, Ahmed Abul Gheit. Ziara hiyo inafanyika katika wakati muhimu, Abul Gheit ameliambia gazeti la al-Ahram, siku ya Jumamosi, kwa sababu upande wa Marekani unakaribia kutangaza mtazamo wake juu ya njia ya kufikia amani na kumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni ambaye alichukua nafasi ya rais Mubarak mwezi Mei wakati rais huyo alipoamua kutofanya ziara iliyopangwa nchini Marekani , baada ya kifo cha mjukuu wake, ni sehemu pia ya ujumbe wa Misr kwa ajili ya ziara hii, pamoja na mkuu wa masuala ya kijasusi nchini Misr, na mawaziri wa fedha, biashara na habari.

Misri inasimamia mazungumzo ya upatanishi kati ya chama kinachoungwa mkono na mataifa ya magharibi cha Fatah na watawala wa katika eneo la ukanda wa Gaza, chama cha Hamas, lakini hadi sasa si juhudi hizo ama jaribio la kuanzisha mazungumzo kati ya Israel na Palestina yaliyopiga hatua kubwa.

Mwandishi Sekione Kitojo /AFPE

Mhariri : Othman Miraj.

 • Tarehe 17.08.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JD2O
 • Tarehe 17.08.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JD2O

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com