1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Gbagbo kuwekewa vikwazo

Kabogo Grace Patricia20 Desemba 2010

Vikwazo hivyo vya kimataifa vitawekwa dhidi ya Rais wa Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo na maafisa wake 18.

https://p.dw.com/p/Qglv
Rais wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo, akiwa na mkewe Simone.Picha: AP

Jumuiya ya kimataifa imetishia kumuwekea vikwazo Rais aliye madarakani nchini Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo pamoja na maafisa wake 18 kutokana na kitendo chake cha kukataa kukubali kuwa ameshindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo mwezi uliopita. Jumuiya ya kimataifa inamtambua kiongozi wa upinzani, Alassane Ouattara kuwa ndiyemshindi wa uchaguzi huo.

Shinikizo la kimataifa la kumtaka Rais Laurent Gbagbo kuachia madaraka linazidi kupamba moto, huku ghasia kati ya pande mbili pinzani zikiongezeka ambapo hadi sasa watu 50 wameuawa tangu Alhamisi iliyopita. Ufaransa, Marekani, Umoja wa Ulaya na Canada, zimetishia kuweka vikwazo hivyo. Maja Kocijancic, msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema kuwa wanadiplomasia wa umoja huo leo wamekubaliana kuhusu majina ya watu ambao watawekewa vikwazo vya kusafiri katika nchi za Umoja wa Ulaya na mali zao kuzuiliwa.

Watu hao 19, mbali na Rais Gbagbo ni mkewe, Simone pamoja na mlinzi wake. Wengine ni washauri wa rais, maafisa wa ngazi ya juu wa usalama, maafisa wa jeshi na mkuu wa kituo cha televisheni ya taifa. Hatua hiyo itaanza kutekelezwa katika muda wa saa 48 zijazo.

Akizungumza baada ya mkutano wa Umoja wa Ulaya Ijumaa iliyopita, Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa alisisitiza kuwa Rais Gbagbo hana jinsi, isipokuwa kuachia madaraka haraka iwezekanavyo. Katika hatua nyingine mkuu wa kikosi cha jeshi cha Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire, leo ameushutumu utawala wa Rais Gbagbo kwa kufanya vitendo visivyokubalika dhidi ya wanadiplomasia wa kigeni, kuwabugudhi wanajeshi wa kulinda amani na kuvuruga shughuli za kusambaza mahitaji yao.

Naye mratibu wa shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa kanda ya Afrika Magharibi, Mutoye Mobiala ameelezea juu ya ripoti za kuweko visa vya ukiukaji wa haki za binaadamu vinavyofanywa na vyombo vya usalama.

Akizungumza na Deutsche Welle Bwana Mobiala alisema, ''Tumepokea kutoka kwa tawi letu la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire ripoti kuhusu vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu kuhusu idadi ya watu kadhaa waliouawa pamoja na kuandamwa kwa wale wanaotuhumiwa walimuunga mkono Bwana Ouattara kwenye uchaguzi.''

Hata hivyo, Rais Gbagbo hajaonyesha dalili zozote za kuachia madaraka na badala yake anajaribu kujiimarisha akiungwa mkono na jeshi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,AFPE, DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman