1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush awasili Israel kusheherekea miaka 60 ya kuundwa kwa taifa hilo.

Mohamed Dahman14 Mei 2008

Rais George W. Bush wa Marekani aanza ziara ya kuzitembelea Israel,Saudi Arabia na Misri kushinikiza mchakato wa amani wakati umwagaji damu ukiendelea.

https://p.dw.com/p/Dzj6
Rais George W. Bush wa Marekani akikaribishwa kwa furaha na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion mjini Tel Aviv leo hii.Picha: AP

Rais George W . Bush wa Marekani amewasili Mashariki ya Kati leo hii kusheherekea miaka 60 ya kuundwa kwa taifa la Israel na kujaribu kuupa nguvu mchakato wa amani ambao umekuja kugubikwa na kashfa ya rushwa ambayo inaweza kumuondowa madarakani Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.

Rais Bush amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion mjini Tel Aviv na kukaribishwa na Waziri Mkuu Ehud Olmert na Rais Shimon Perez.

Bush atahudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa kwa taifa la Israel kufuatia maangamizi ya Wayahudi milioni 6 mikononi mwa Manazi wa Ujerumani.Sherehe hizo zinafanyika mjini Jerusalem leo na kesho.

Shughuli yake ya kwanza itakuwa ni kukutana na Waziri Mkuu Olmert na Rais Perez.

Kuendelea kwa machafuko katika eneo hilo kunaweka kiwingu kwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Wapalestina ambayo hayakuwa na maendeleo makubwa ya maana tokea yafufuliwe upya katika mkutano ulioandaliwa na Bush nchini Marekani hapo mwezi wa Novemba kufuatia kukwama kwa mchakato huo kwa miaka saba.

Hata hivyo kabla ya kuwasili Israel Bush ameelezea matumaini yake ya kufikikwa kwa makubaliano ya amani kabla ya yeye kundoka madarakani hapo mwezi wa Januari mwaka 2009 licha ya umwagaji damu unaoendelea huko Gaza na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi huko Ukingo wa Magharibi.

Bush amesema amekuja kutanabahi kwamba ni muhimu kwa Israel kuwa mshirika wa Palestina ambalo litakuwa taifa la kidemokrasia lililojizatiti kwa amani nafahamu fika kwamba Wapalestina wote wanakubaliana na lengo hilo lakini pia anaamini kwamba wakati wote mtu anapokabiliwa na hali hiyo ya maisha huko Gaza na kunapozushwa changamoto kwa amani Wapalestina wengi watachaguwa amani.

Katika ziara yake hiyo Bush atalihutubia bunge la Israel na kutembelea magofu ya ngome ya Masada ambayo yamekuja kuwa alama ya ushujaa wa Wayahudi baada ya madarzeni ya Wayahudi kuamuwa kujiuwa wenyewe mahala hapo kuliko kusalimu amri kwa Waroma katika mwaka wa 70 baada ya kuzaliwa Yesu Kristo.

Matukio hayo mawili yatafanyika hapo kesho siku ambayo Wapalestina watakuwa na kumbukumbu ya kukimbia kwa mamia na maelfu ya Waarabu ambao walipoteza makaazi yao na ardhi zao wakati taifa la Israel lilipoundwa hapo mwezi wa Mei mwaka 1948.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert hapo jana amesema maendeleo ya kweli yamefikiwa katika mazungumzo na Wapalestina kwamba maelewano na makubaliano yamefikiwa katika masuala muhimu kabisa.

Olmert amesema wanataka kuamuwa kwa dhati bila ya kusita sita licha ya matatizo yote yalioko licha ya vitisho vilioko na licha ya kutokuwa na uhakika kulifanya taifa la Israel lifikie amani pamoja na upinzani na maadui ili kukomesha umwagaji damu wanaoushuhudia tokea kuundwa kwa taifa la Israel na hata kabla ya hapo.

Wakati huo huo waziri mkuu huyo wa Israel amekuwa akizidi kukabiliwa na wito wa kumtaka ajiuzulu kutokana na madai ya kupokea hongo kutoka kwa mfadhili wa Marekani.Wapalesina wana wasi wasi kwamba sakata hilo la Olmert linaweza kuifanya Israel ichukuwe msimamo mkali zaidi kuhusiana na suala la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi na kupelekea kupamba moto kwa mapambano ya kijeshi na hiyo kukwamisha zaidi mazungumzo yoyote yale ya amani.

Kikwazo chengine ni kuendelea kwa umwagaji damu katika Ukanda wa Gaza unaotawaliwa na kundi la Hamas ambapo Israel mara kwa mara imekuwa ikiendesha operesheni zake za kijeshi na kuuwekea vikwazo vyenye madhara makubwa leo hii Wapalestina wanne wameuwawa katika operesheni hizo za kijeshi za Israel.

Katika ziara yake hii Bush hatokanyaga ardhi ya Wapalestina na badala yake atakutana na Rais Mahmoud Abbas wa Wapalestina huko Sharm el- Sheikh nchini Misri hapo Jumamosi na Jumapili.

Mbali na Misri ziara hiyo ya Bush pia itamfikisha Saudi Arabia.