Rais Bush awaaga Wamarekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Bush awaaga Wamarekani

Amtakia kila jema rais anayeingia madarakani Barack Obama

default

Rais wa Marekani George W. Bush (kulia) na rais mteule Barack Obama

Rais wa Marekani George W Bush ametoa hotuba yake ya mwisho kuliaga taifa. Katika hotuba hiyo aliyoitoa jana, rais Bush amesema licha ya kupitisha maamuzi yaliyozusha utata wakati wa utawala wake, kunaweza tu kuwa mjadala mdogo kwamba maamuzi hayo yameilinda Marekani na kuwa salama. Rais Bush anatazamwa kuwa rais mwenye sifa mbaya anayeondoka madarakani huku umaarufu ukiwa umeshuka kufikia chini ya asilimia 30.

Rais Bush alikuwa pamoja na familia yake, marafiki zake wa kisiasa, wafanyakazi na Wamarekani waliomuunga mkono, wakati alipokuwa akitoa hotuba yake ya mwisho kuliaga taifa katika ikulu ya mjini Washington.

Kiongozi huyo alizungumzia mada nyingi alizozishuhgulikia wakati wa utawala wake wa miaka minane katika hotuba hiyo. Aliwakumbusha Wamarekani kuhusu mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 katika miji ya New York na Washington yaliyowaua watu takriban 3,000, akiyaeleza kuwa mashambulio mabaya kuwahi kutokea tangu mashambulio ya Pearl Harbour.

Zaidi ya miaka saba tangu mashambulio hayo, rais Bush ameonya kuwa ugaidi bado kitisho kikubwa kinachowakibili Wamarekani, akisisitza kuwa maadui wana subira na wameamua kuishambulia tena Marekani. Amesema Marekani ndio nchi pekee inayoweza kuongoza juhudi za kutafuta uhuru na demokrasia ulimwenguni kote na kupigana na ugaidi. Ndio maana amevieleza vita vya Afghanistan na Irak kuwa na umuhimu mkubwa.

''Afghanistan imebadilika kutoka taifa ambako wapiganaji wa Taliban waliwahifadhi wanamgambo wa al Qaeda na kuwapiga mawe wanawake, na kuwa demokrasia changa inayopiga vita ugaidi na kuwahimiza wasichana kwenda shule. Irak imeondokana na udikteta katili na kuwa demokrasia ya kiarbu katikati mwa Mashariki ya Kati na rafiki wa Marekani.''

Kuhusu maswala ya ndani ya Marekani, rais Bush alifaulu kupitisha kiwango kikubwa cha fedha kuusaidia uchumi wa Marekani ambao umeporomoka. Marekani inakabiliwa na wakati mgumu na itaendelea kukabiliwa na hali hiyo iwapo hatua muafaka hazitachukuliwa. Licha ya kuyumba kwa uchumi wa Marekani rais Bush amesema anaamini mambo yatakuwa mazuri na uchumi utainuka na kuendelea kukua.

''Kwa dhamiri na kufanya kazi kwa bidii tutaunusuru uchumi wentu uendelee kukua tena. Tutauodhihirishia ulimwengu kwa mara nyingine tena uthabiti wa mfumo huru wa uchumi wa Marekani.''

Kusambaratika kwa masoko ya fedha na kukaribia kufilisika kwa kampuni kubwa za kutengeza magari za Marekani hakujaubadili msimamo wake rais Bush kuhusu biashara huru. Rais Bush anaondoka madarakani akiwa hana wasiwasi kuhusu hali ya uchumi na amesema alifanya kila alichoweza.

Wakati wa hotuba yake kwa Wamarekani rais Bush hakusita kujikosoa mwenyewe kwa kusema changamoto zilizomkabili zilimlazimu kupitisha maamuzi ambayo pengeine hayakuwafurahisha Wamarekani wengi.

''Kama walionitangulia katika wadhifa huu , nimekabiliwa na changamoto na kuna mambo ambayo ningeyafanya tofauti kama ningepewa nafasi. Nimekuwa nikiyajali maslahi ya nchi yetu. Nimefuata dhamira yangu na kufanya nilichodhani ni sawa. Pengine hamtakubaliana na baadhi ya maamuzi magumu niliyopitisha, lakini natumaini mnaweza kukubali nilikuwa tayari kupitisha maamuzi hayo.''

Rais Bush amesisitiza kwamba historia utauhukumu utawala wake unaomalizika Jumanne ijayo wakati Barack Obama atakapoapishwa saa sita mchana. Obama anachukua hatamu za uongozi wakati uchumi ukiwa katika hali mbaya na vita vinavyoendelea nchini Irak na Afghanistan. Rais mteule Barack Obama pia anarithi kazi ambayo haijaisha ya kuifunga jela ya Guantanamo Bay nchini Cuba.

Rais Bush amemtakia kila la kheri Barack Obama akisema historia ya Obama inadhihirisha ahadi ya ndoto ya Marekani.

 • Tarehe 16.01.2009
 • Mwandishi Charo Josephat / Albrecht Ziegler
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GZo4
 • Tarehe 16.01.2009
 • Mwandishi Charo Josephat / Albrecht Ziegler
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GZo4
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com