1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Buhari kuzuru Niger Delta

1 Juni 2016

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria Alhamisi (02.06.2016) kwa mara ya kwanza tokea aingie madarakani mwaka mmoja uliopita atatembelea eneo la Niger Delta ambalo linasibiwa na mashambulizi dhidi ya vituo vya mafuta na gesi.

https://p.dw.com/p/1IyRI
Picha: picture-alliance/dpa/W. Krumm

Ziara hiyo inakuja wakati kundi la wanamgambo wanaojiita walipa kisasi wa Niger Delta ambalo limedai kuhusika na mfululizo wa mashambulizi ya hivi karibuni likitowa onyo kwa makampuni ya mafuta katika eneo hilo la kusini mwa Nigeria kwamba vituo vya mafuta pamoja na wafanyakazi wao watakabiliwa na ghadhabu za kundi hilo.

Buhari hapo Jumapili amesema serikali itakuwa na mazungumzo na viongozi wa mkoa huo wenye kuzalisha mafuta kwa wingi nchini Nigeria kuyapatia ufumbuzi manun'guniko yao katika juhudi za kuzuwiya kuongezeka kwa mashambulizi ya mabomba ya mafuta.

Katika ziara hiyo Buhari atatembelea eneo linaloitwa Ogoniland ili kuzinduwa mpango iliochelewa mno kuanza wa kusafisha maeneo yaliochafuliwa sana na uvujaji wa mafuta.

Mpango wa kusafisha Ogoniland

Joe Westby wa Shirika la haki za binaadamu la kimataifa la Amnesty ambalo limekuwa likifanya kampeni ya muda mrefu kudai kusafishwa kwa eneo hilo ni hivi karibuni tu amerudi kutoka Ogoniland na ameelezea umuhimu wa operesheni hiyo kwa Niger Delta na Nigeria kwa jumla.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria hapo Alhamisi (02.06.2016) kwa mara ya kwanza tokea aingie madarakani mwaka mmoja uliopita atatembelea eneo la Niger Delta ambalo linasibiwa na mashambulizi dhidi ya vituo vya mafuta na gesi na atazinduwa opereseheni iliokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya kusafisha eneo lililochafuliwa na uvujaji wa mafuta.
Ogoniland eneo lilioathirika na uvujaji wa mafuta huko Niger Delta.Picha: picture-alliance/dpa/M. van Dijl

Amesema " Umoja wa Mataifa ulibainisha katika repoti yake kuu hapo mwaka 2011 jinsi watu katika eneo la Ogoniland wanavyoishi katika mazingira yaliochafuliwa na uvujaji wa mafuta maisha yao yote.Wameshuhudia njia za kujikimu kimaisha zikiangamizwa kwamba watu hawawezi tena kulima au kuvua.Hali ni mbaya kiasi kwamba watu inabidi wanywe na kuoga katika maji ambayo yamechafuliwa na vitu vya sumu inayotokana na mafuta."

Repoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa mazingira (UNEP) ilisema eneo la Ogoniland yumkini likahitaji operesheni kubwa kabisa kuwahi kufanyika duniani ya kulisafisha eneo hilo ambapo imekadiriwa zingelihatajika dola bilioni moja katika operesheni hiyi itakayodumu kwa takriban miaka 30.

Malalamiko ya wakaazi

Wakaazi katika maeneo ya vinamasi ya kusini mwa Nigeria ambapo kampuni za mafuta za Royal Dutch Shell na Chevron yanaendesha shughuli zake wamekuwa wakilalamika kwa miaka mingi juu ya uchafuzi unaofanywa na kampuni hizo na kuhusu kutengwa kiuchumi na serikali.

Wapiganaji wa Niger Delta.
Wapiganaji wa Niger Delta.Picha: picture-alliance/dpa

Baadhi yao wamebeba silana na kufanya mashambulizi dhidi ya vituo vya nishati jambo lililopelekea kushuka kwa uzalishaji wa mafuta kufikia kiwango cha chini kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 20.

Suala liliopo je Rais Buhari ana nia ya kisiasa na nguvu kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.Akijibu suala hilo Westby wa Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu la Amnesty amesema "Kwa hakika amejitolea kulisafisha eneo hilo na ameashiria hayo kwa haraka mara tu baada ya kuingia madarakani kwa maafisa wake kulitembelea eneo hilo na kuzungumza na jamii zilizoathirika lakini hatua hizo zinatakiwa zitafsiriwe kwa vitendo kwa kuyasafisha maji na kuyarudisha mazingira katika hali yake ya kwaida".

Maafisa wa eneo hilo na washirika wa mataifa ya magharibi kama vile Uingereza wamemwambia Buhari kupeleka wanajeshi pekee katika eneo hilo la Delta hakuwezi kuzuwiya mashambulizi na kwamba kinachohitajika ni kushughulikia kwanza manun'guniko ya wananchi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri : Iddi Sessanga