Rais Bouteflika wa Algeria ajiandaa kugombea kipindi cha tatu | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.12.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Bouteflika wa Algeria ajiandaa kugombea kipindi cha tatu

mgawanyiko katika kambi ya upinzani kumfagilia njia.

default

Rais AbdelAziz Bouteflika

Mgawanyiko katika kambi ya upinzani nchini Algeria, unaelekea kumnufaisha Rais Abdelaziz Bouteflika ambaye baada ya marekebisho ya katiba yanayoondoa kifungu cha mihula miwili ya madaraka ya Rais, yanamfungulia nafasi kiongozi huyo kugombea tena mwakani 2009.

Kuwania tena Urais kwa mhula wa tatu baada ya marekebsho ya katiba yaliofanyika tarehe 12 mwezi huu wa Novemba na kuzusha wimbi la malalamiko kutoka kambi mbali mbali za kisiasa nchini humo, sasa kunaonekana kuwa ni jambo lenye uwezekano mkubwa kwa Rais Bouteflika mwenye umri wa miaka 71.

Bouteflika yumo katika miezi ya mwisho mwisho ya kipindi chake cha uongozi ambacho kama si marekebisho hayo kingekua cha mwisho kwa mujibu wa katiba.

Kutokana na hayo kambio ya upinzani imo mbioni kumtafuta mgombea atakayekubalika ili kuleta mabadiliko na kumaliza utawala wa Bouteflika.

Lakini bado mgombea huyo hajapatikana na kizingiti kwa sehemu ni kuwa pande zinazohusika zinashindwa kukubaliana katika masuala kadhaa likiwemo linalohusiana na jninsi ya kukabiliana na rushwa. Baadhi ya wapinzani ambao ni wa itikadi za Kiislamu wanataka Algeria yenye wakaazi milioni 34 itawaliwe kwa misingi ya sheria na maadili ya utamaduni wa Kiislamu.

Moja kati ya majina yanayotokeza katika kumsaka jitihada za kumsaka mgombea anayekubalika ni lile la Lamine Zeroual mwanajeshi mkakamavu aliyewahi kuwa rais kuanzia 1994-1999.

Akiwa ni mtu anayeheshimiwa na wazalendo huenda asikubalike kwa waislamu, hasa kwa kuwa kipindi chake cha uongozi kiliandamana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, serikali dhidi ya wakundi ya kiislamu. Mpaka sasa hajatamka lolote juu ya wito unaomtaka agombee.

Wengi katika kambi ya upinzani wamevunjwa moyo kwa sababu wanaamini huenda Bouteflika amepata uungaji mkono wa kundi la wanajeshi wenye usemi linalojulikana " kama Le Pouvoir" yaani Utawala ambalo limetawala siasa za Algeria tangu uhuru.

vigogo hawa wenye umri kati ya miaka ya 60 na sabaini na kitu na ambao wamo katika nyadhifa kadhaa za madaraka ni wale ambao ni maveterani wa vita dhidi ya ukoloni wa kifaransa 1954-1962. Na kutokana na mchango wao wana nafasi maalum katika jukwaa la kisiasa ambazo hawataki kuona zikiwatoka.

Gazeti moja lilimnukuu Waziri mkuu Ahmed Ouyahia ambaye anakiongoza chama kimoja cha kisiasa kinachoonekana kuwa karibu na jeshi, akisema " upinzani hautoingia kamwe madarakani nchini Algeria."

Wachambuzi wanasema wanasiasa wa upinzani wanaonekana pengine wanaweza kusimama dhidi ya Bouteflika wanatoka katika vyama dhaifu vya kisiasa ambavyo si kitisho hata kidogo kwa watawala.

Wengi wanategemea upinzani utaususia uchaguzi huo kwa lengo la kuhujumu uhalali wa Bouteflika kugombea tena. Lakini wachambuzi wanasema vyovyote itakavyokua, wengi miongoni mwa Algeria, kilio chao ni kile kile ,lazima yafanyike mabadiliko kuboresha maisha yao. Wanahitaji makaazi, ujenzi wa shule mpya, hospitali mpya na kadhalika,ikiwa na maana pato la utajiri wa mafuta na gesi litumike kuinua hali za maisha za Waalgeria. Kwa sasa wanaitwika dhamana serikali na mtawala wa sasa Bouteflika kwa hali ngumu wanayokumbana nayo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com