1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bashir wa Sudan kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu

Thelma Mwadzaya4 Machi 2009

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita,ICC imetangaza kutolewa hati ya kimataifa ya kukamatwa Rais wa Sudan Omar al Bashir kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/H5h7
Rais wa Sudan Omar al BashirPicha: AP Photo


Hata hivyo pendekezo la Mwendesha mashtaka mkuu Louis Moreno Ocampo la kumtia kiongozi huyo hatiani kwa tuhuma za mauaji ya halaiki zimetupuliwa mbali na mahakama hiyo.Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi aliye madarakani kushtakiwa na mahakama hiyo tangu kuasisiwa kwake mwaka 2002.

Mahakama hiyo ya ICC ilitangaza kuwa Rais Omar al Bashir wa Sudan anakabiliwa na mashtaka 7 ya kuhusika na uhalifu wa kivita vilevile dhidi ya ubinadamu.Hati hiyo kadhalika imetupilia mbali pendekezo la mwendesha mashtaka Louis Moreno Ocampo la kumtia hatiani kiongozi huyo kwasababu ya tuhuma za kuhusika na mauaji ya halaiki kama anavyosisitiza Silvana Araba Msajili wa Mahakama ya ICC.''Majaji wamewasilisha hati katika kitengo cha usajili dhidi ya Omar Hassan Ahmed Al Bashir kuhusiana na mashtaka ya uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu.Hati hiyo haijumuishi mashtaka ya kuhusika na mauaji ya halaiki kama ilivyopendekezwa na mwendesha mashtaka.''

Ombi hilo lilitolewa mwezi Julai mwaka uliopita.

Rais Omar al Bashir anashtakiwa kwa kuhusika na harakati za kupambana na uasi katika eneo la Darfur magharibi mwa Sudan kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano hadi mwaka 2008.Mashambulizi hayo yanaripotiwa kuzilenga jamii za Fur,Masalit na Zaghawa.Hata hivyo mahakama hiyo imeeleza kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kuwa serikali ya Rais al Bashir ilinuia kuzitendea unyama jamii hizo.Laurence Blairon ni msemaji wa mahakama ya uhalifu wa kivita ICC na anaelezea kuwa''Mahakama hii ilibaini kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuthibitisha kuwa serikali ilinuia kuziangamiza jamii za Fur,Masalit na Zaghawa.''

Hata hivyo mahakama hiyo imeeleza kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kuwa serikali ya Rais al Bashir ilinuia kuzitendea unyama jamii hizo. Rais Al Bashir anatuhumiwa kwa kuwaagiza wanajeshi wa serikali walioungwa mkono na wapiganaji wa Janjaweed walio na asili ya Kiarabu kuwashambulia wakazi wa eneo la Darfur.

Maafisa wa mahakama hiyo kwa upande mwengine wamesisitiza kuwa endapo ushahidi wa ziada utabatili hilo kesi hiyo itatilia maanani suala hilo.Rais Al-Bashir ni kiongozi wa kwanza wa taifa aliye madarakani kushtakiwa na mahakama ya ICC kadhalika tangu kuasisiwa kwake mwaka 2002.Uamuzi wa mahakama hiyo umetolewa wakati ambapo hofu ya ghasia kuzuka imetanda nchini Sudan.

Rais Al Bashir kwa upande wake amekanusha mashtaka hayo na kupuuzilia mbali uamuzi uliotolewa na mahakama ya ICC.Kwa upande wake serikali ya Sudan kupitia naibu Waziri wa Mambo ya kigeni Ali Ahmed Kart inapinga vikali uamuzi huo kadhalika madai ya mwendesha mashtaka mkuu ya tuhuma za mauaji ya halaiki.Uongozi huo ulionya kuwa endapo hati ya kukamatwa kwa Rais Al Bashir itaidhinishwa Sudan itavunja uhusiano wake na Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa mshauri wa Rais Bashir Mustafa Osman Ismail hatua hiyo haikuwashtua na ina lengo la kuliyumbisha taifa la Sudan

Umoja wa Afrika AU kwa pamoja na Umoja wa nchi za Kiarabu Arab League wametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati kuzuia hati hiyo kutolewa kwasababu mazungumzo ya amani bado yanaendelea nchini Sudan.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia wa ngazi za juu kauli hizo zimeungwa mkono na Urusi na China.Ifahamike kuwa nchi tatu wanachama wa kudumu wa Baraza hilo Marekani,Ufaransa na Uingereza zina mtazamo tofauti.

Wakati huohuo kundi la waasi la Darfur la Justice and Equality Movement JEM limepongeza hatua hiyo.Kulingana na msemaji wao Mohammed Hussein Sharif aliyeko mjini Cairo nchini Misri tukio hilo ni la kihistoria na wanamtolea wito Rais Bashir kuthibitisha kuwa hana hatia kwa kujibu mashtaka yanayomkabili.

Mamia ya wakazi wa Khartoum wanaropotiwa kuandamana nchini Sudan punde baada ya tangazo la mahakama ya ICC kutolewa.Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa wito wa amani kudumishwa ili kuzuia umwagikaji zaidi wa damu.

Mwaka 2005 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiagiza mahakama ya ICC kuchunguza hali katika eneo hilo la Darfur.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa yapata watu alfu 35 wameuawa kwenye eneo la Darfur tangu mwaka 2003 na wengine laki 3 wamefariki kwasababu ya njaa na magonjwa.Kiasi cha watu milioni 2.7 wameachwa bila ya makazi kwasababu ya vita hivyo.

AFPE

RTRE





Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi