Rais Bashir kujua hatima yake na ICC | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 14.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Rais Bashir kujua hatima yake na ICC

Ban Ki-moon ana wasiwasi na athari za hatua za Ocampo

Luis Moreno Ocampo,wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya Jinai

Luis Moreno Ocampo,wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya Jinai

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai- ICC anafichua jumatatu ushahidi aliyonao wa uchunguzi kuhusiana na ukatili uliofanywa katika mkoa wa Sudan wa Darfur,na wanadiplomasia wanatamtarajia kumfungulia mashtaka ya mauaji ya halaiki pamoja na makosa dhidi ya binadamu kiongozi wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir.

Mwanadipolomasia wa Ulaya wa ngazi za juu alisema Ijumaa iliyopita kuwa mwendesha mashtaka mkuu Luis Moreno-Ocampo anaweza akaomba kutolewa hati ya kumkamata rais Omar Hassan al-Bashir kwa madai ya kuhusika katika ukatili dhidi ya watu wa mkoa wake wa Darfur.

Ikiwa hatua hiyo, ambayo inatarajiwa kuanza muda mchache kutoka sasa mjini The Hague Uholanzi itafanikiwa hii ndiyo itakuwa mara ya kwanza kwa kiongozi aliye madarakani kutaka kukamatwa na mahakama hiyo, tangu mwaka wa 2003 wakati aliposhtakiwa kiongozi wa zamani wa Liberia Charles Taylor.

Lakini taarifa iliyotolewa kupitia Televisheni ya taifa ya Sudan imesema kuwa chama cha rais Bashir cha National Congress Party kimeonya jana kuwa ,endapo rais Omar Hassan al-Bashir atashtakiwa ,kile kilichoita umwagikaji zaidi wa damu na ghasia vitalikabili eneo la magharibi mwa nchi hiyo ambalo ni Darfur.

Makundi muhimu ya waasi wa Sudan ambayo nayo yamelaumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu,yamesema kuwa waranti wa kumkamata Bashir ukitolewa utakuwa ufanisi wa haki na sheria na kuapa kuwa yatawakabidhi makamanda wao ikiwa watahitajika na mahakama hiyo.

Serikali ya Sudan ikiwa inapinga hatua ya mwendesha mashtaka imesema kuwa hatua hiyo itavuruga juhudi za mchakato wa amani wa Darfur.

Athari za amani ya Darfur pia zimeguswa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki -moon.Amesema kuwa alizungumza kwa simu na rais Bashir jumamosi na kukariri uhuru wa mahakama hiyo,huku akiongeza kuwepo kwa haja ya kudhibiti hali ya mambo katika eneo la Darfur.Aidha ana wasiwasi ya majaliwa ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa huko.

Sudan inataraji msaada wa kuzuia waranti hiyo kupitia marafiki zake kama vile China,Urusi pamoja na mataifa mengi ya Kiafrika katika kikao cha baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

Serikali ya Sudan inasema haiitambui mahakama hiyo.Rais Bashir anaripotiwa jana kufanya kikao maaluma cha baraza lake la mawaziri kutafakari hatua ya leo ya mahakama ya ICC dhidi yake.Pia baraza hilo linasemekana lilijadili majibu ya hatua ya mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya uhalifu wa kivita.

Pia Sudan imeomba kufanyika kikao cha dharura cha mawaziri wa mashauri ya kigeni wa umoja wa nchi za kiarabu wa Arab League .

Yeye rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh amenukuliwa kusema kuwa hatua yoyote ya ICC ya kuwashtaki maafisa wa serikali ya Sudan itakuwa kama kupalilia chuki,vurugu pamoja na kuwasha moto zaidi katika eneo hilo.

Rais wa Yemen amenukuliwa na shirika la habari la Sudan akilaani hatua hiyo aliyoiita ya undumila kuwili.

Na ikiwa hatua ya leo jumatatu ya mwendesha mashtaka mkuu Luis Moreno-Ocampo itakubaliwa na majaji wa mahakama hiyo,itakuwa mara ya kwanza kwa mahakama hiyo kumfungulia mashtaka rais alioko madarakani.Hata hivyo viongozi wengine kama vile Slobodan Milosevic wa Serbia na Charles Taylor wa Liberia nao waliweza kushtakiwa na makosa ya uhalifu wa kivita.

Tangu mwaka wa 2003 inakisiwa watu takriban laki tatu wanasemekana kuuawa katika ghasia za kikabila katika eneo la Darfur na wengine millioni 2 kukosa makazi yao na hivyo kugeuka wakimbizi.

Mgogoro wa Darfur ulianza pale raia wake weusi walipoanzisha vita dhidi ya serikali ya Khartoum wakipinga kile wanachosema kama kunyanyaswa.

Serikali ya Sudan inalaumiwa kwa kujibu ikitumia wanamgambo wa Janjaweed ambao wanasemekana walitenda mauaji.

Umoja wa mataifa mwaka wa 2003 uliiamuru mahakama ya ICC kufanyika uchunguzi.

 • Tarehe 14.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ec9n
 • Tarehe 14.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ec9n
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com