Rais Banda abatilisha uchaguzi Malawi | Matukio ya Afrika | DW | 24.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Banda abatilisha uchaguzi Malawi

Rais Joyce Banda wa Malawi Jumamosi (24.05.2014) ameutangaza uchaguzi wa wiki hii wenye vurugu kuwa "batili na haufai" na kutaka ufanyike uchaguzi mpya hatua ambayo inaitumbukiza nchi hiyo ya kimaskini kwenye mgogoro.

Rais Joyce Banda wa Malawi.

Rais Joyce Banda wa Malawi.

Banda ambaye alidai kwamba kulikuwako na "dosari kubwa" za uchaguzi huo amesema uchaguzi mpya unapaswa kufanyika katika siku zisizozidi 90 lakini amesema hatosimama kama mgombea katika uchaguzi huo ili kuwapa nafasi wananchi wa Malawi kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.

Katika kauli aliyoitowa kupitia radio amesema "Kama rais natumia madaraka niliyopewa na katiba kuutangaza uchaguzi huo kuwa batili na haufai."

Hata hivyo Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) imepinga tangazo hilo la Rais Banda kubatilisha uchaguzi huo wa Malawi.

Mwenyekiti wa (MEC) Maxon Mbendera ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba kwa kadri anavyofahamu rais hana madaraka yoyote yale ya kikatiba kubatilisha uchaguzi kwamba ni tume ya uchaguzi ndio yenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Ombi la Banda la kutaka kukaguliwa kwa matokeo ya uchaguzi huo limepuuzwa na mwenyekiti huyo wa tume ya uchaguzi ambaye ameliambia shirika la habari la AFP kwamba licha ya kuwepo kwa matatizo katika mfumo wa kuhesabu kura kwa njia ya elektroniki kura hizo zinaendelea kuhesabiwa kwa mkono.

Mbendera amesisitiza kwamba uchaguzi huo unafaa na kwamba madai ya Banda ni ishara ya kutapatapa.

Dosari kubwa

Amesema anashauriana na mwanasheria mkuu wa serikali kuhusu agizo hilo la rais.Kulikuwa na vurumai katika kituo cha kuhesabu matokeo ya kura za uchaguzi huo mjini Blantyre wakati habari zilipoanza kusambaa kwamba uchaguzi huo umebatilishwa ambapo polisi iliamuru kufungwa kwa kituo hicho.

Rais Joyce Banda wa Malawi akipiga kura yake.

Rais Joyce Banda wa Malawi akipiga kura yake.

Banda amedai kwamba watu walipiga kura zaidi ya mara moja, kura zilitiwa mkono,maafisa waliokuwa wakisimamia uchaguzi walitiwa mbaroni na mfumo wa kuhesabu kura kwa njia ya kompyuta ulisambaratika.

Wafuasi wake wanadai mpinzani wake mkuu Peter Mutharika ambaye tayari alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya uhaini kabla ya uchaguzi huo yumkini akawa na mkono wake kutokana na dosari za uchaguzi.

Awali walisema hawatakubali kushindwa baada ya matokeo ya awali kuonyesha kwamba alikuwa amepitwa sana akiwa ameshikilia nafasi ya pili.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa Ijumaa usiku na tume ya uchaguzi wakati theluthi moja ya kura zikiwa zimehasabiwa Mutharika mwenye umri wa miaka 74 alikuwa na asilimia 42 wakati Banda alikuwa na asilimia 23.

Mutharika apinga kubatilishwa uchaguzi

Peter Mutharika (katikati) mwenye miwani mpinzani mkuu wa Rais Banda wa Malawi.

Peter Mutharika (katikati) mwenye miwani mpinzani mkuu wa Rais Banda wa Malawi.

Mutharika ni kaka wa Rais Bingu wa Mutharika aliefariki wakati akiwa madarakani miaka miwili iliopita.Ilidaiwa kuwa alijaribu kuficha kifo cha kaka yake huyo kwa kuusafirisha mwili wake Afrika Kusini katika jaribio la kumzuwiya Banda wakati akiwa makamo wa rais kuingia madarakani kama inavyoamuru katiba jambo ambalo ndio lililopelekea kufunguliwa kwa mashtaka ya uhaini dhidi yake.

Mutharika amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna msingi wa kisheria kuzuwiya uchaguzi huo na kwamba wamegeuka kichekesho kwa hiyo ni vyema kadri uchaguzi huo utakapomalizika na mapema.

Mutharika amemtaka kiongozi huyo wa Malawi kuachana na njia itakayoitumbukiza nchi hiyo kwenye ghasia wakati wafuasi wake wakiandamana na kufanya fujo katika kiunga cha Limbe nje ya Blantyre kupinga agizo hilo la rais.

Baada ya utawala wa Mutharika wa miaka minane uliohusishwa na rushwa ,Banda alipokewa vizuri na mataifa ya magharibi akiwa kama miongoni mwa viongozi wachache wa kike barani Afrika na hata kumpokea aliekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani wakati huo Hillary Clinton katika ziara yake ya Malawi iliopigiwa upatu mkubwa.

Kashfa ya "cashgate"

Zoezi la kupiga kura Malawi.

Zoezi la kupiga kura Malawi.

Lakini serikali yake ikaja kuhusishwa katika kashfa ya rushwa ya dola milioni 30 iliopachikwa jina la "cashgate" ambayo imesababisha wafadhili wa kigeni wasitishe msaada unaohitajika mno na nchi hiyo.Msaada huo yumkini ukaendelea kusitishwa kwa kadri mgogoro wa nchi hiyo utapokuwa unaendelea.

Uchaguzi wa nchi hiyo ulikuwa umepangwa ufanyike Jumanne lakini uliongezewa muda hadi Alhamisi lakini kuchelewa kuanza kwa uchaguzi huo kwa hadi saa 10 kulizusha fujo katika mji mkuu wa kibiashara wa Blantyre ambapo jeshi imebidi litumike.

Rais Banda aliiomba mahakama kuu kuzuwiya kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi lakini mahakama hiyo imekataa kufanya hivyo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP/Reuters

Mhariri : Caro Robi