Rais apendekeza achaguliwe na wananchi | Magazetini | DW | 26.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Rais apendekeza achaguliwe na wananchi

Suala moja lililozingatiwa ni pendekezo ambalo rais Köhler wa Ujerumani alilitoa. Kwenye mazungumzo ya televisheni, Rais huyu alitaja wazo lake la kuwa rais wa nchi hii achaguliwe na wananchi wenyewe badala na hadhara kuu ya wawakilishi wa rais kama ilivyo hivi sasa.

Pendekezo hilo limezusha mjadala mkubwa juu ya mfumo wa uchaguzi. Wengi wa wahariri wa magazeti wana wasiwasi juu ya kuubadilisha mfumo kama ulivyo sasa, kama vile gazeti la “Märkische Allgemeine” la mjini Potsdam lilivyoandika:

“Kisheria ingetoa picha kama demokrasia itaimarishwa ikiwa rais wa taifa atachaguliwa moja kwa moja na wananchi. Kwa kweli, lakini, si hivyo. Mfumo wa mamlaka katika taifa la shirikisho umepimwa vizuri ili kupata usawa. Wadhifa wa rais ni kuwawakilisha wananchi kwenye sherehe rasmi. Ikiwa anapewa mamlaka, itakuwa ni serikali nyingine ambayo inadhoofisha mamlaka ya Kansela na bunge.”

Katika gazeti la “Süddeutsche Zeitung” tunasoma pia wasiwasi juu ya pendekezo hilo la rais Köhler:

“Kiti hiki cha rais ni bahati kubwa kwa taifa. Yule anayetaka kufanyika uchaguzi wa urais, lazima ampe rais mamlaka zaidi. Lakini hakuna anayejua vipi kumpa mamlaka zaidi. Usawa wa nguvu utaathirika iwapo mwingine mwenye mamlaka atakuwepo.”

Ni gazeti la “Süddeutsche Zeitung”. Anayemuunga mkono rais Köhler ni mhariri wa “Nordbayerischer Kurier”. Naye ameandika:

“Muda umewadia tuthubutu kufanya kitu kipya. Uchaguzi wa moja wa moja wa rais ungekuwa ni ishara muhimu ya kuanza upya na kuimarisha msingi wa demokrasia, yaani mamlaka yapo kwa wananchi.”

Twende katika suala la pili ambalo linalozungumziwa leo kwenye kurasa za maoni ya wahariri, nalo ni maendeleo katika Mashariki ya Kati na mkutano wa Sharm el-Sheikh. Ufuatao ni uchambuzi wa gazeti la “Frankfurter Allgemeine”:

“Wakati mkutano wa Sharm el-Sheikh ulikuwa bado ukiandaliwa, mtu anayechukua nafasi ya pili katika uongozi wa kundi la Al-Qaida, Zawahiri, alitoa mwito wa kuliunga mkono kundi la Hamas katika eneo la ukanda wa Gaza. Zawahiri anataka kulipa nguvu kundi la Hamas na kulitumia silaha nyingi zaidi. Kwa hivyo, inabidi kufanya kila iwezekanavyo kulizuia eneo la Gaza, ambalo wengi wanaliita “Hamastan” siku hizi, lisiwe kama makao makuu ya magaidi.”

Na mwishowe tunalinukuu gazeti la “Coburger Tageblatt” ambalo linasema hakuna njia nyingine ila tu kuzungumza na Hamas.

“Hadi sasa, Wapalestina hawajapatiwa fursa ya kuunda taifa lao. Sasa lakini kuna uwezekano wa kuwepo hata mataifa matatu, yaani Israel, ukanda wa Gaza na eneo la Magharibi mwa mto Jordan. Ili kuzuia hali hii isitokee, itaibidi Israel izungumze na Hamas. Kisiasa haiwezekani kutolijali kundi lenge nguvu kama Hamas. Inaaminika kuwa kisirisiri tayari kuna mahusiano fulani kati ya Israel na Hamas. Huenda yatasaidia kupunguza uchungu na kuliokoa eneo la Gaza.”

 • Tarehe 26.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSb
 • Tarehe 26.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSb