1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Abbas hatakutana na Pence kutokana mzozo wa Jerusalem

9 Desemba 2017

Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahamud Abbas hatakutana na Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence atakapokuwa ziarani Mashariki ya Kati baada ya Marekani kutangaza kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

https://p.dw.com/p/2p4Vp
USA Mahmud Abbas & Donald Trump in Washington
Picha: Reuters/C. Barria

Mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa Rais Abbas, Majdi al Khaldi amesema hakutakuwa na mkutano kati ya Abbas na Pence ndani ya Palestina kwa sababu Marekani imevuka mstari mwekundu kwa kuchukua uamuzi wa kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kupanga kuhamishia ubalozi wake huko.

Ikulu ya Rais wa Marekani ya Marekani ilikuwa imeonya siku ya Alhamisi kuwa kufutilia mbali mkutano uliokuwa umepangwa kati ya Abbas na Pence katika ukingo wa Magharibi baadaye mwezi huu ni jambo lisilo na manufaa.

Uamuzi wa Trump waughadhabisha Ulimwengu

Lakini Abbas amelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya uamuzi uliochukuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump ambao umelaaniwa vikali na nchi za Kiislamu na Jumuiya ya kimataifa.

Jerusalem US-Präsident Trump Benjamin Netanjahu
Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/Zuma/M. Stern

Jibril Rajoub mwanachama mwandamizi wa chama cha Abbas cha Fatah alishasema siku ya Jumatano, Trump alipochukua uamuzi huo wa kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel kuwa Pence hakaribishwi Palestina.

Makamu huyo wa Rais wa Marekani anatarajiwa kuizuru Israel na Palestina kabla ya sherehe za Krismasi. Palestina imesema Marekani haiwezi tena kuwa mpatanishi wa amani katika mzozo wa muda mrefuu wa Mashariki ya Kati.

Takriban watu wanne wameuawa baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga katika kambi ya kijeshi ya Nusseirat iliopo katikati ya mji wa Gaza. Kambi hiyo ya kijeshi ni ya kundi la Hamas.

Siku ya Ijumaa, askari wa Israeli walikabiliana na maelfu ya Wapalestina waliokuwa wanaandamana kupinga hatua ya Rais Trump ya kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israeli.

Mamlaka ya Israeli na nchi jirani za Mashariki ya Kati zinahofia kuzuka kwa maandamano zaidi na vurugu. Watu wapatao 760 walijeruhiwa  katika vurugu za Ijumaa. Majeshi ya Israel yameongeza doria katika maeneo ya Jerusalem, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Kutambua Jerusalem kutayapa makundi ya itikadi kali nguvu

Katika mkutano wa dharura ulioitishwa siku ya Ijumaa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani imeshutumiwa vikali na wanachama wengine wa Baraza hilo. Balozi wa Misri katika Umoja wa Mataifa Amr Abdellatif Aboulatta amesema uamuzi wa Marekani wa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israeli itasababisha msukosuko.

Deutschland Proteste in Berlin gegen Anerkennung Jerusalems als Israels Hauptstadt
Waandamanaji wapinga uamuzi wa Trump kuhusu JerusalemPicha: Getty Images/S. Gallup

Mabalozi wa Uingereza, Italia, Uswisi na Ujerumani, walitoa taarifa ya pamoja baada ya mkutano huo, wamesema uamuzi wa Marekani hauendani na maazimio ya Umoja wa Mataifa na wala hauna manufaa.

Baada ya sala ya Ijumaa nchi nyingi za Kiislamu, kama vile Misri, Jordan, Lebanon, Indonesia na Tunisia zilishuhudia maandamano ya watu waliokuwa wanapinga uamuzi huo wa Rais Trump.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu Anwar Gargash amesema uamuzi huo wa Marekani unayapa nguvu makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali akiongeza mambo kama hayo ya kuchukua maamuzi hatari na ya kichokozi ni kama zawadi kwa makundi hayo, ambayo wanachama wake watatumia kama kisingizio kueneza chuki duniani.

Korea Kaskazini ambayo kiongozi wake Kim Jong Un amekuwa wakirushiana cheche za maneno na Trump imemtaja Kiongozi huyo wa Marekani kuwa aliyepungukiwa na akili kwa kuchukua uamuzi huo wa kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel ambao umesema ni uamuzi wa hatari na unaokusudia kuzua maovu.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Zainab Aziz