1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Abbas amfuta kazi waziri mkuu Haniya

15 Juni 2007

Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amechagua waziri mkuu mpya baada ya kiongozi huyo kumuachisha kazi waziri mkuu wa zamani Ismail Haniya.

https://p.dw.com/p/CB3Z
Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas
Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud AbbasPicha: AP

Kwa mujibu wa msaidizi wa rais Mahmoud Abbas waziri wa fedha Salam Fayyad ndie wazairi mkuu mpya wa Palestina.

Bwana Fayyad mwanasiasa asiyelemea upande wowote na anaeheshimiwa sana na jamii ya kimataifa atachukuwa mahala pa aliyekuwa waziri mkuu Ismail Haniya baada ya kusimamishwa kazi na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas mara tu chama chake cha Hamas kilipoudhibiti mji wa Gaza kimabavu.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice amesema kuwa rais Abbas ametumia uwezo wake wa kisheria.

Wakati huo huo ujumbe wa usalama na wafanyakazi waliokuwa wakiiwakilisha Misri katika Ukanda wa Gaza umeondoka kutoka mjini humo kwa mujibu wa shirika la habari la Ma’an la Palestina.

Misri iliwaitisha wawakilishi wake hao pamoja na wawakilishi wa kidiplomasia kutoka Ukanda wa Gaza leo hii.

Balozi wa Misri katika maeneo ya Palestina Ashraf Aqel anatarajiwa kuondoka kutoka katika Ukanda wa Gaza jioni hii kufutia hali inayozidi kuzorota ya usalama.

Jenerali Muhammad Burhan aliyeongoza ujumbe wa kiusalama wa Misri katika Ukanda wa Gaza na aliyekuwa mpatanishi kwa muda mrefu kati ya Hamas na Fatah ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ameshaondoka kutoka mjini Gaza.

Jenerali, huyo amefahamisha kuwa yuko mjini Cairo kujadili na serikali ya Misri juu ya hali ya kisiasa na usalama iliyopo katika Ukanda wa Gaza.

Umoja wa Ulaya umesema unamuunga mkono rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas katika hatua anazochukua kukabiliana na mzozo wa eneo hilo.

Ujerumani ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa umoja huo imezitaka nchi wanachama na pande zote kumuunga mkono kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.

Kamishna wa uhusiano wa nje wa umoja wa ulaya Benita Ferrero-Waldner amemtaja rais Mahmoud Abbas kuwa ndie rais wa haki kwa Wapalestina.

Mapigano ya hivi karibuni yamesababaisha mgawanyiko katika eneo la Palestina, kwa sasa eneo la Ukanda wa Gaza liko chini ya udhibiti wa chama cha Hamas chenye uhusiano na Utawala Syria na Iran huku eneo la Ukingo wa Magharibi likiwa chini ya udhibiti wa chama cha Fatah chenye uhusiano na Israel na nchi za magharibi.