1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila odinga apanga mikutano zaidi ya hadhara Kenya

Shisia Wasilwa
3 Februari 2023

Tume ya Uwiano na Utangamano imemtaka kiongozi huyo kusitisha mikutano hiyo kwa hoja kwamba italiyumbisha taifa.

https://p.dw.com/p/4N3Pf
Kenia Präsidentschaftswahl | Raila Odinga
Picha: John Ochieng/Zuma/IMAGO

Muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya ukiongozwa na Raila Odinga unapanga mikutano ya hadhara inayolenga kujadili masuala mazito yanayoiathiri Kenya, huku Tume ya Uwiano na Utangamano ikimtaka kiongozi huyo kusitisha mikutano hiyo kwa hoja kwamba italiumbisha taifa hilo linalojaribu kusimama tena baada ya uchaguzi mkuu ulioshuhudia ushindani na upinzani mkali.

Odinga: Nitamuondoa Ruto madarakani

Katika kipindi cha majuma mawili, Raila ameandaa mikutano miwili ya hadhara jijini Nairobi, na wafuasi wake wanasema kuwa ndio mwanzo wa ngoma…Mikutano hiyo ikilenga kuishinikiza serikali ya rais William Ruto kuleta mageuzi pamoja na kupunguza gharama za maisha ambazo zimepanda si haba.

Chibukati atishia 'kumburuza' Raila mahakamani

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, kiongozi wa wachache kwenye bunge la taifa Opiyo Wandayi amesema kuwa Azimio la Umoja litaanda mkutano mwingine katika mtaa wa Kibra ambao ni ngome ya siasa ya Raila, punde tu kiongozi huyo wa upinzani atakaporejea nchini kutoka Afrika Magharibi.

Katika kipindi cha majuma mawili, Raila ameandaa mikutano miwili ya hadhara jijini Nairobi, na wafuasi wake wanasema kuwa ndio mwanzo wa ngoma
Katika kipindi cha majuma mawili, Raila ameandaa mikutano miwili ya hadhara jijini Nairobi, na wafuasi wake wanasema kuwa ndio mwanzo wa ngomaPicha: Shisia Wasilwa/DW

Raila amekuwa akiyapinga matokeo ya Uchaguzi uliofanyika Agosti 2022

Juma moja baadaye, mkutano mwingine wa hadahara utafanyika katika jimbo la Machakos, huku wafuasi wao wakitakiwa kufika kwa wingi na kwa utele...Tangu kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka uliopita, Raila ameyapinga matokeo hayo, licha ya mahakama ya Juu zaidi nchini Kenya kuthibitisha ushindi wa Ruto.

Viongozi wa dini Kenya wapewa kibarua cha kurejesha umoja

Hatua ya Raila ikionekana kuupa upinzani nguvu, baada ya kunyongonyea katika utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Jeremiah Kioni ni Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee kinachoegemea upande wa Azimio.

"Tutampa upinzani unaostahiki. Upinzani unaoweza kumuondoa mamlakani, kwenye ofisi aliyomo kinyume cha sheria. Baadaye tutaanda mikutano hiyo katikati ya juma. Tutajadili ahadi walizowapa Wakenya,” amesema Jeremiah Kioni.

Ikumbukwe kuwa Rais Ruto amekamilisha miezi mitatu tu, tangu achaguliwe kuwa rais. Upinzani unasema kuwa mikutano hiyo ya hadhara itakuwa sawa na ile iliyoandaliwa mwaka 2016, iliiyochangia kutimuliwa kwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wakati huo Isaack Hassan.

Kenya: Wito wa kuunda afisi ya kiongozi wa upinzani

Ni masuala yapi upinzani unataka ushughulikiwe?

Baadhi ya masuala ambayo upinzani unataka serikali iyaangazie ni pamoja na kuongezeka kwa gharama za maisha pamoja na uteuzi wa makamishna wa tume ya kusimamia uchaguzi na mipaka. Kaunti nyingine ambapo upinzani unajiandaa kufanya mikutano ni pamoja na Kakamega, Kiambu, Nakuru, Isiolo, Kisumu, Mombasa, Kisii, Turkana na Garissa.

Hayo yanajiri huku Tume ya Uwiano na Utangamano ikimtaka Raila kusitisha mikutano hiyo kwa kile inachokitaja ni kupandisha joto la siasa nchini. 

Hata hivyyo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanahisi kuwa hatua ya upinzani, huenda ikasababisha ghasia nchini kwani Ruto alichaguliwa kuwa rais kwa njia ya sheria.

Mara ya mwisho kwa maandamano kama hayo kufanyika kwenye serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, matokeo yake yalikuwa salamu za heri, hata hivyo Rais Ruto amesimama kidete akisema kuwa, hatashirikiana na Raila kwenye serikali yake.