Raia zaidi ya 30 wauwawa mashariki ya Congo | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.08.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Raia zaidi ya 30 wauwawa mashariki ya Congo

Jeshi la Congo limesema Jumapili (14.08.2016) kwamba takriban raia 36 wameuwawa katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambalo limekumbwa na matumizi ya nguvu tokea mwaka 2014.

Msemaji wa jeshi Mak Hazukay ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watuhumiwa waasi wa kundi la Allied Demokratic Forces (AFD) ambalo ni kundi la Waislamu wa itikadi kali wenye asili yao nchini Uganda limeuwawa "watu 36" katika mji wa Beni Jumamosi usiku.

Amesema "ndio kwanza wamegunduwa miili yao."katika kitongoji cha Rwangoma kwenye viunga vya mji wa Beni na kwamba miili zaidi inaendelea kutafutwa.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi waasi hao wa ADF wameweza kukwepa maeneo waliyoko majeshi ya serikali na kuweza kuingia katika maeneo walioko raia na kuwauwa katika kulipiza kisasi kwa jili ya operesheni za kijeshi zinazofanyika katika eneo hilo.

Gilbert Kambale kiongozi wa shirika la kiraia katika eneo hilo amesema shambulio hilo limetokea kati ya saa moja usiku na saa tano za usiku hapo Jumamosi na kwamba tayari kulikuwa na miili 35 katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Beni.

Kambale amesema kuna hasira kubwa sana kutokana na kushindwa kwa serikali kurudisha usalama katika eneo hilo na kwamba inatia wasi wasi kutokana na kwamba rais wa jamhuri alikuwako katika eneo hilo na halafu yanakuja mauaji hayo.

Beni yaathirika zaidi

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo alipokutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo alipokutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Mauaji hayo mapya yamepelekea maandamano makubwa yaliyojaa ghadhabu ambapo watu wanaofikia mia moja wametoka mitaani na kauli mbiu za kuipinga serikali na kudai usalama.

Mauaji hayo yametokea siku tatu baada ya Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kuutembelea mkoa huo na kuahidi kufanya kila awezalo kuleta amani na usalama katika eneo hilo.

Beni iko katika Mkoa wa Kivu Kaskazini jimbo ambalo limeshuhudia mfululizo wa mashambulizi ambayo serikali na Umoja wa Mataifa inalialumu kundi hilo la ADF kwa kuhusika nayo.

Hususan eneo la Beni limekuwa likishuhudia mauaji kadhaa tokea mwaka 2014 ambayo kwa jumla yamepelekea zaidi ya raia 600 kupoteza maisha yao.

Mauaji yazusha maandamano

Jeshi la Congo katika operesheni dhidi ya waasi wa AFD.

Jeshi la Congo katika operesheni dhidi ya waasi wa AFD.

Wakati wa mchana takriban waandamanaji 100 waliokuwa wameubeba mwili wa mmojawapo wa wahanga walikusanyika mjini wakipiga mayowe ya ghadhabu dhidi ya Kabila na serikali yake.

Mwanaharakati wa haki za binaadamu katika eneo hilo Jackson Kesereka amesema wakaazi kaskazini mwa mji huo walikuwa wakiunguza matairi barabarani kupinga mauaji hayo na kuonyesha hasira yao kwa serikali.

Kwanza wakaazi wa eneo hilo waliwadhania waasi hao kuwa ni wanajeshi kabla ya kuanza kushambuliwa kwa mapanga na kupigwa risasi.Shambulio hilo linasemekana kuwa la kikatili kabisa kuwahi kufanywa na waasi wa ADF mwaka huu.

Hivi karibuni Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo alikutana na kiongozi mwenzake wa Uganda,Yoweri Museveni na kuzungumzia ushirikiano katika mapambano dhidi ya waasi wa ADF ambao wanampinga Rais Museveni na wamekuwepo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa zaidi miaka 20.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Hamidou Oummilkheir

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com