1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wayemen wakabiliwa na kitisho cha njaa

Admin.WagnerD28 Julai 2015

Kutokana na mapigano na mashambulizi ya kutokea angani ya miezi kadhaa raia wa Yemen wanakabiliwa na kitisho cha baa la njaa. Shirika la misaada la Oxfam limeonya juu ya kutokea janga kubwa la kibinaadamu nchini humo.

https://p.dw.com/p/1G5hB
Hunger im Jemen
Wachuuzi sokoni Sanaa wanaouza vyakula wakila miraaPicha: AP

Miezi minne tangu kuongezeka kwa machafuko nchini Yemen shirika la Oxfam limesema kuna uwezekano mkubwa wa kutokea janga la kibinaadamu lisilo mithili. Shirika hilo linasema tangu harakati ya kijeshi dhidi ya waasi wa Houthi inayofanywa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ilipoanza mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa imeongezeka kufikia 25,000 kwa siku.

Hadi sasa idadi jumla ni watu milioni 13 – ikiwa ni nusu ya idadi jumla ya wakaazi wa Yemen. Kwa mujibu wa Oxfam kila mtu mmoja kati ya wawili huenda akakabiliwa na njaa, kama hali ya usambazaji wa mahitaji ya msingi haitaboreka.

Idadi kubwa ya watu ambayo haijawahi kushuhudiwa hawana chakula. Shirika la Oxfam linasema watu wengi wanateseka katika taifa hilo kutokana na njaa, iliyosababishwa na mapigano yasiyokoma na hatua ya kuizingira na kuifunga nchi hiyo yanayofanywa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia. Yemen hutegemea sana misaada na huagiza kutoka nje asilimia 80 ya mahitaji muhimu ya chakula. Lakini tangia mwezi Machi ni asilimia 20 tu ya chakula ambacho kimefika nchini humo.

Mkurugenzi wa shirika la Oxfam nchini Yemen, Philippe Clerc, amesema licha ya kitisho cha kutokea janga kubwa la kibinaadamu pande zinazopigana zinapuuza miito yote inayotolewa ya kutaka mapigano yasitishwe. Mbali na mabomu na risasi zinazofyetuliwa kila upande raia vile vile hawafahamu watakula nini wala kukipata wapi chakula.

Hunger im Jemen
Mwanamume wa Yemen akinywa maji kutoka mfuko wa plastiki nje ya msikiti SanaaPicha: AP

Shirika la Oxfam linasema hali ni mbaya zaidi katika ngome ya waasi wa Houthi katika mkoa wa kaskazini wa Saada, ambako kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa asilimia 80 ya watu wanakabiliwa na njaa mkoani humo.

Bei zaongezeka kwa asilimia 274

Kwa mujibu wa Oxfam uhaba wa chakula umesababisha bei za vyakula kupanda kwa asilimia hadi 274. Wakaazi wengi hawana kipato tena tangu miezi kadhaa iliyopita. Utafiti uliofanywa na shirika la Oxfam katika mkoa wa Hajjah unaonesha familia nyingi ambazo zimelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, zimeuza mifungo yao kwa thamani ya chini katika soko, ili ziweze kununua chakula na vitu vingine muhimu kwa ajili ya maisha yao. Hii ni ishara ya kutisha.

Waasi wa Houthi walifaulu kuudhibiti mji mkuu Sanaa mwezi Januari mwaka huu wakisaidiwa na sehemu ya jeshi. Waliposonga mbele kuelekea mji wa bandari wa kusini wa Aden, rais wa Yemen Abed Rabbo Mansur Hadi aliikimbia nchi kwenda Saudi Arabia kutafuta msaada. Ufalme wa Saudi Arabia ndipo ukaanza mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya waasi hao katika harakati inayozijumuisha nchi nyingine za kiarabu, kwa lengo la kuwafurusha waasi wa Houthi kutoka mjini Sanaa na kumrejesha madarakani rais Hadi.

Muungano huo ulitangaza Jumapili iliyopita usitishwaji wa mapigano kwa sababu za kibinaadamu, lakini saa chache baadaye baada ya usitishwaji huo kuanza kutekelezwa, mashambulizi yakaanza tena.

Mwandishi:Josephat Charo/dw.com/deutsch

Mhariri:Daniel Gakuba