Raia 7 wa kigeni wauwawa Nigeria | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.03.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Raia 7 wa kigeni wauwawa Nigeria

Italia na Ugiriki zimethibitisha kuwa raia saba wa kigeni waliotekwa nyara kutoka kampuni moja ya ujenzi mwezi uliopita na kundi haramu la Ansaru nchini Nigeria wameuwawa.

Kundi la kigaidi la Anasaru lawauwa raia wa kigeni Nigeria

Kundi la kigaidi la Anasaru lawauwa raia wa kigeni Nigeria

Kundi lililo na mafungamano na mtandao wa al-Qaida, Ansaru, siku ya Jumamosi lilitangaza kuwa liliwauwa raia saba kutoka mataifa ya kigeni waliowateka nyara tarehe 7 mwezi uliopita katika jimbo liliko kaskazini la Bauchi kwa sababu ya majaribio ya majeshi ya Nigeria na Uingereza kuwaokoa.

Kundi hilo lilichapisha picha zinazoonyesha miili ya raia wa Uingereza, Italia, Ugiriki na wafanyakazi wanne wa kutoka Lebanon waliotekwa nyara kutoka majengo ya kampuni ya Kilebanoni.

Nigeria bado haijathibitisha vifo

Hadi jana, mataifa ambayo raia wake walitekwa yalikuwa hayajaweza kuthibitisha mauaji hayo. Italia na Ugiriki zimekanusha kuwa kulikuwa na jaribio lolote la serikali zao kuwaokoa mateka. Serikali ya Nigeria nayo haijaweza kuthibitisha mauaji hayo kufikia sasa.

Waziri wa mambo ya nje wa Italia Giulio Terzi

Waziri wa mambo ya nje wa Italia Giulio Terzi

Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia inasema kuwa wanaamini kuwa taarifa za kijasusi walizozipokea pamoja na mataifa mengine husika, zinathibitisha kuwa habari za kuuwawa kwa mateka hao ni za kweli na kuongeza kuwa rais wa Italia ametuma risala za rambirambi kwa familia ya raia wa Italia aliyeuwawa.

Afisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imetoa jina la raia wake aliyeuawa kama Brendan Vaughan. Taarifa za kijasusi kutoka Nigeria zinasema raia wa Italia, Silvano Trevisan, alikuwa na matatizo ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo.

Hali ya usalama imekuwa mashakani katika kampuni za mafuta na miundo mbinu katika kanda hiyo ya magharibi mwa Afrika tangu wanamgambo wanaofunagamana na mtandao wa al-Qaida kuvamia kiwanda kimoja cha gesi nchini Algeria mwezi Januari na kuwauwa karibu raia 37 wa kigeni katika jaribio la jeshi la Algeria kuwaokoa.

Jeshi la Ufaransa nchini Mali

Jeshi la Ufaransa nchini Mali

Hatari imeongezeka zaidi katika mataifa ya magharibi na kaskazini mwa Afrika tangu Ufaransa itume majeshi yake nchini Mali kudhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo iliyo ngome ya waasi wenye mafungamano na al-Qaida.

Makundi ya kigaidi yazidi kuwa tisho

Makundi ya kigaidi pia yameenea kaskazini na eneo la kati mwa Nigeria ambako kuna utajiri mkubwa wa mafuta na kuwa tisho kwa usalama wa taifa hilo. Utekaji nyara hasa unaolenga raia wa kigeni si jambo geni katika eneo hilo kwa miaka mingi na makundi yanayoteka nyara hudai kulipwa kitita cha fedha kabla ya kuwaachilia huru mateka wao, lakini katika siku za hivi karibuni mkondo umebadilika na matokeo yake ni vifo.

Kundi hilo la Ansaru mnamo mwezi Januari lilitangaza kutengana na Boko Haram lakini maafisa wa usalama wanaamini kuwa bado ni kitu kimoja. Ansaru limeshukiwa kutekeleza visa vya hivi karibuni katika eneo la kaskazini mwa Nigeria na Uingereza tayari imeliorodhesa kama kundi la kigaidi.

Maafisa wa usalama wa Nigeria bado wanaitafuta familia moja ya watu saba kutoka Ufaransa iliyotekwa nyara kaskazini mwa Cameroon na kuingizwa Nigeria na waasi wa Boko Haram.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com