1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia 33 wauawa Syria katika mashambulizi

John Juma
22 Machi 2017

Raia 33 wauawa Syria karibu na mji wa al-Raqqa, kufuatia mashambulizi yanayoaminika kufanywa kwa ndege za vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani. Mashambulizi hayo yalilenga shule moja ambayo wakimbizi wamekuwa wakiishi.

https://p.dw.com/p/2ZhqG
Syrien Konflikt 7. August 2013
Picha: Abdullah Al-Sham/AFP/Getty Images

Watu 33 wameuawa karibu na mji wa al-Raqqa nchini Syria, kufuatia mashambulizi ya  kutokea angani yanayoaminika kufanywa kwa ndege za vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani. Kundi la uangalizi la haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza limesema.

Mashambulizi hayo yalilenga shule iliyoko magharibi ya mji wa al-Raqqa ambayo wakimbizi wanaishi. Mji wa al-Raqqa ni ngome kuu ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Syria.

Haya yanajiri wakati maafisa wakuu kutoka nchi 68 ambazo zinashirikiana dhidi yawakitarajiwa kukutana jijini Washington Jumatano, kujua mengi kuhusu mpango wa Rais Trump kutaka kuziangamiza ngome za wapiganaji wa Jihadi ambazo zimesalia nchini Syria na Iraq.

Ndege ya kivita ya vikosi vinavyopiga vita IS
Ndege ya kivita ya vikosi vinavyopiga vita ISPicha: picture-alliance/AP Images/C. Ena

Mashambulizi hayo yalifanyika usiku wa Jumatatu, lakini taarifa kuhusu idadi ya waliouawa zilijulikana baadaye. Likiwanukuu wakaazi, kundi hilo la uangalizi la haki za binadamu limesema familia 40 ambazo ziliyakimbia makazi yao katika maeneo ya al-Raqqa, Homs na Aleppo walikuwa wakiishi katika shule iliyoshambuliwa.

 

Raia wengi wauawa

Kundi hilo limeongeza kuwa idadi ya waliokufa kufuatia mashambulizi ya vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani katika vijiji vya al-Raqqa tangu tarehe 8 mwezi Machi sasa imefikia raia 116, miongoni mwao watoto 18.

Vikosi hivyo vilianzisha mashambulizi ya angani dhidi ya makundi ya wapiganaji wa Jihadi nchini Syria mwezi Septemba mwaka 2014. Al-Raqqa ni mji uliodhibitiwa na kundi la IS tangu mwaka 2014. Mnamo Novemba mwaka uliopita, wapiganaji wa kundi la Kikurdi walioungwa mkono na Marekani walianzisha mashambulizi ya kuukomboa mji huo kutoka kwa kundi la IS. Katika miezi ya hivi karibu kundi la IS limepata pigo kubwa kijeshi na kupoteza ngome zake nchini Syria na nchi jirani ya Iraq.

Wapiganaji wa IS mjini Raqqa
Wapiganaji wa IS mjini RaqqaPicha: picture-alliance/AP Photo

Mapema mwezi huu, muungano wa vikosi dhidi ya IS ulisema mashambulizi yake nchini Syria na Iraq yalisababisha vifo vya raia 220 kwa bahati mbaya. Lakini makundi mengine ya uangalizi yanasema idadi ni zaidi ya hiyo.

Zaidi ya watu 320,000 wameuawa na mamilioni wamepoteza makazi yao tangu vita vya Syria vilipoanza mwezi Machi mwaka 2011. Vita hivyo vimechangia kuibuka kwa makundi ya wapiganaji wa Jihadi na kusababisha vikosi vya kimataifa kushiriki. Rais wa Marekani Donald Trump amewaamuru majenerali wake wakuu kuandaa mkakati wa kulitokomeza kundi la IS.

Mwandishi: John Juma/DPAE/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu