1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar yapata kiongozi mpya

25 Juni 2013

Qatar imepata kiongozi wake mpya, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, ambaye amechukuwa madaraka kutoka kwa baba yake, tukio ambalo ni la nadra sana kwenye mataifa ya Kiarabu.

https://p.dw.com/p/18vUE
Qatar's Crown Prince Sheikh Tamim Bin Hamad al-Thani attends the closing ceremony of the 12th Arab Games at Al-Sadd Stadium in Doha, in this December 23, 2011 file picture. Qatar's Emir Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani said on June 25, 2013 he was stepping down and handing power to his son Sheikh Tamim, explaining it was time for a new generation to take over. REUTERS/Fadi Al-Assaad/File (QATAR - Tags: SPORT ROYALS)
Katar Kronprinz Tamim bin Hamad al-ThaniPicha: Reuters

Saudi Arabia, taifa jirani, la kifalme na ambalo limeendelea na utamaduni wa wafalme wake kuzeekea na kufia madarakani, limekuwa la kwanza kutoa salamu za pongezi kwa kiongozi huyo kijana, mwenye umri wa miaka 33 tu, likisema limefurahishwa na hatua hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Saudia, SPA, Mfalme Abdullah ametuma ujumbe maalum kwa Sheikh Tamim.

"Kwa niaba ya watu, Ufalme na serikali ya Saudi Arabia, tuna furaha ya kukupongeza kwa dhati. Tuna imani utaendeleza safari ya baba yako na juhudi zake za kulitumikia taifa la Qatar na watu wake na pia kuimarisha mahusiano kati ya mataifa yetu mawili." Amesema Mfalme Abdullah.

Hatua iliyotangazwa leo na baba yake Sheikh Tamim, Amir Hamad bin Khalifa al-Thani, inamaliza wiki kadhaa za uvumi. Licha ya kutokutoa maelezo zaidi katika tangazo lake, wadadisi wanaamini kwamba Sheikh Hamad, mwenye umri wa miaka 61, ana matatizo ya kiafya.

Sasa Sheikh Tamim, ambaye alisomea nchini Uingereza, ataanza utaratibu wa kuunda serikali mpya ambayo wengine wanaamini itakuwa tafauti sana na nyengine zenye mawaziri wengi wazee, miongoni mwa mataifa yanayoungwa mkono na Magharibi.

Hapatarajiwi mageuzi ya kisera

Hata hivyo, kiongozi huyo anayechukua hatamu ya taifa lenye utajiri wa mafuta na gesi na pia ushawishi wa kisiasa kwenye eneo hilo, hatarajiwi kufanya mabadiliko yoyote ya haraka kwenye siasa za nje.

Kiongozi wa Qatar aliyeondoka madarakani, Hamad bin Khalifa al-Thani.
Kiongozi wa Qatar aliyeondoka madarakani, Hamad bin Khalifa al-Thani.Picha: AFP/Getty Images

Wakosoaji wanaituhumu Qatar kutumia utajiri wake mkubwa kujijenga kisiasa ndani ya eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, jambo ambalo limechochea uasi na mabadiliko ya uongozi kwenye baadhi ya mataifa hayo.

Ni Qatar iliyojitokeza kuwaunga mkono wazi wazi waasi wa Libya dhidi ya Muammar Gaddafi na sasa inawaunga mkono waasi wa Syria dhidi ya utawala wa Bashar al-Assad.

Pia iliwahi kugombana na mataifa mengine ya Ghuba kwa kulisaidia kundi la Udugu wa Kiislamu, lililosambaa eneo hilo zima, na ambalo sasa limeingia madarakani nchini Misri.

Nchi hiyo imejitokeza pia kama msuluhishi kati ya makundi hasimu ya Wapalestina na kwenye mgogoro wa Darfur, nchini Sudan.

Kiongozi wa Qatar hujuilikana kwa jina la Amir na Sheikh Tamim, ambaye alichukua nafasi ya urithi baada ya kaka yake mkubwa kujiondoa mwaka 2003, anatarajiwa kuendeleza mafanikio ya baba yake, kwani tangu hapo alikuwa mshauri mkubwa wa baba yake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf