1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin na Kim wakutana kwa mara ya kwanza

Admin.WagnerD25 Aprili 2019

Rais wa Urusi Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wamekutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza wote wawili wakiahidi kuimarisha mahusiano ya karibu yanayonuwia kukabiliana na ushawishi wa Marekani. 

https://p.dw.com/p/3HOpy
Russland Wladiwostok Treffen Putin und Kim
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Mkutano baina ya viongozi hao wawili katika mji wa mashariki ya Urusi wa Vladivostok umekuja wakati Kim anajaribu kukabiliana na Marekani kuhusiana na mpango wake wa nyuklia na wakati Putin analenga kuifanya Urusi kuwa taifa la mstari wa mbele kwenye mvutano huo.

Viongozi hao wawili walipeana mikono na kutabasamu kabla ya kuelekea kwenye mazungumzo ya faragha yaliyodumu kwa muda wa saa mbili.

Kwenye taarifa fupi iliyotolewa kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Kim na Putin walisema wanalenga kuimarisha mahusiano baina yao kwa kiwango sawa na enzi za Muungano wa zamani wa Kisovieti ambao ulimuunga mkono kiongozi mwasisi wa Korea Kaskazini na babu wa Kim, hayati Kim Ill Sung.

Kim amesema anatumai kubadili mahusiano ya sasa na Urusi kuwa imara na yenye mashiko wakati Putin amesema ziara ya Kim inakoleza mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kwa mataifa hayo mawili.

Wote wawili waahidi mahusiano zaidi

Russland Wladiwostok Treffen Putin und Kim
Picha: Reuters/Sputnik/A. Nikolsky

Wakati wanadiplomasia kutoka pande zote mbili walipojiunga na viongozi hao kwa mazungumzo ya ngazi ya juu Kim alisema "Ndugu Rais, tumekuwa na mazungumzo ya manufaa na ya ana kwa ana kuhusu masuala ya maslahi yetu ya pamoja na matatizo yetu ya sasa. Nakushukuru sana kwa muda uliotenga.”

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza kwa Kim na kiongozi wa nchi nyingine tangu aliporejea kutoka mkutano wa Hanoi, Vietnam na rais wa Marekani Donald Trump mnamo mwezi Februari ambao ulivunjika bila ya kufikia makubaliano kuhusu kuukongoa mfumo wa silaha za nyuklia wa nchi yake.

Rais Putin  amesema suala la hali ya usalama kwenye rasi ya Korea ilikuwa sehemu ya ajenda za mazungumzo yao, "Bila shaka, tumezungumia hali kwenye rasi ya korea na tumebadilishana mawazo juu ya vipi na nini kinapaswa kufanywa kuimarisha hali iliyopo kwa ajili ya siku bora za baadae."

Kim amechagua diplomasia badala ya ubabe

Russland Nordkorea l Treffen von  Vladimir Putin und Kim Jong Un - Ankunft
Picha: Reuters/Press Service of Administration of Primorsky Krai/A. Safronov

Tangu Machi 2018 kiongozi wa Korea Kaskazini amekwishafanya mikutano minne na rais wa China, mitatu na rais wa Korea Kusini pamoja na miwili na rais Trump.

Wakati wa mkutano na Trump, Marekani ilisema makubaliano hayakufikiwa kwa sababu Korea Kaskazini ilitoa masharti ya kuondolewa vikwazo vyote bila kueleza yenyewe itafanya nini kuhusu silaha zake za nyuklia.

Urusi imekwishatoa wito wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini wakati Marekani inaituhumu nchi hiyo kwa kuvikuka madai ambayo Moscow imeyakanusha.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Josephat Charo