1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin na Erdogan waijadili Syria

Lilian Mtono
22 Oktoba 2019

Marais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Vladimir Putin wa Urusi wamekutana mjini Sochi hii leo saa kadhaa kabla ya kumalizika kwa muda wa makubaliano ya siku tano ya kusitisha mapigano kaskazini mwa Syria.

https://p.dw.com/p/3RjAz
Treffen Recep Tayyip Erdogan und Wladimir Putin in Sotschi
Picha: Reuters/S. Chirikov

Mazungumzo baina ya rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Vladmir Putin wa Urusi mjini Sochi yanaonekana kuwa muhimu hususan katika kufanikisha mpango wa kuondolewa wanamgambo wa Kikurdi katika eneo la mpaka kati ya Syria na Uturuki. Rais Putin amesema, "Ninataka kuelezea matumaini kwamba kiwango cha mahusiano kilichofikiwa kati ya Urusi na Uturuki katika nyakati hizi, kitakuwa na nafasi muhimu katika suluhu ya masuala yote ya kikanda yanayojitokeza hadi sasa."

Aidha kwenye mazungumzo hayo rais Erdogan ameonya kwamba ukanda huo unakabiliwa na nyakati ngumu kufuatia mzozo huo wa Syria na katika wakati ambapo muda wa kusitisha mapigano ukielekea ukingoni.

Erdogan amesema anaamini mkutano huo utakuwa na manufaa makubwa kikanda kutokana na nyakati ngumu inazopitia. Ingawa Urusi inapingana na uvamizi wa Uturuki nchini Syria lakini kwa pamoja wanakubaliana kuanzishwa kwa ukanda salama utakaoruhusu raia kupita.

Kabla ya kuondoka Ankara, Erdogan alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari kwamba "leo ni siku ya mwisho kwa wanamgambo hao kuondoka kwenye eneo hilo, na kurudia kauli yake kwamba wataanzisha mashambulizi makali zaidi iwapo ahadi ambayo Marekani iliitoa kwa taifa hilo haitatekelezwa."

Alisema, atajadiliana na Putin kuhusu mustakabali wa miji iliyoko mpakani ya Manbij, Qamishli na Kobane, ambayo Ankara inasema ni maeneo salama yaliyopendekezwa.

Syrien Habeet, Provinz Idlib | Präsident Baschar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-Assad alipovitembelea vikosi vyake vilivyopo Idlib.Picha: picture-alliance/AP Photo/Facebook page of the Syrian Presidency

Rais wa Syria, Bashar al-Assad ambaye kwa mara ya kwanza hii leo amevitembelea vikosi vya serikali vilivyoko Idlib amenukuliwa akimtaja Erdogan kama "mwizi", aliyeiba viwanda, ngano na mafuta kwa kushirikiana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS na hii leo anaiba ardhi" hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali ya Syria, SANA.

Wakati waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer akipendekeza kuanzishwa kwa maeneo salama yatakayodhibitiwa kimataifa nchini Syria, rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amekemea mashambulizi hayo na kuitaka Uturuki kuondoa vikosi vyake. 

Katika hatua nyingine vikosi vya Marekani vilivyoondoka Syria vinaelekea nchi jirani ya Iraq ingawa Iraq yenyewe imesema hii leo kwamba vikosi hivyo havina ruhusu ya kukaa nchini humo.

Urusi imeimarisha nafasi yake katika mzozo wa Syria hususan baada ya Marekani kuwaondoa ghafla wanajeshi wake kaskazinimashariki mwa nchi hiyo wiki mbili zilizopita hatua iliyofungua mlango kwa Uturuki kuanzisha mashambulizi dhidi ya Wakurdi Oktoba 9.