1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin asaini sheria ya kuinyakua asilimia 15 ya Ukraine

Daniel Gakuba
5 Oktoba 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametia saini sheria inayokamilisha mchakato wa kuinyakua asilimia 15 ya eneo la Ukraine, kufuatia kile Urusi ilichokiita ''kura ya maoni'' katika maeneo hayo juu ya kujiunga na Urusi.

https://p.dw.com/p/4HlhX
Russland | Wladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin akisaini sheria ya kuyanyakua maeneo ya UkrainePicha: Dmitry Astakhov/Pool Sputnik Government/AP/picture alliance

Duru kutoka bunge la Urusi mjini Moscow zimethibitisha kuwa Rais Putin amesaini sheria ya kikatiba inayozitambua jamhuri zilizojitangaza za Donetsk na Ruhansk, pamoja na mikoa ya Kherson na Zaporizhzhia kuwa sehemu ya Urusi.

Soma zaidi:Bunge la Urusi laidhinisha unyakuzi wa majimbo manne ya Ukraine

Urusi iliyanyakua maeneo hayo ya mashariki mwa Ukraine baada ya ilichokinadi kama kura ya maoni katika sehemu inazozikalia. Ukraine pamoja na nchi za magharibi ziliipinga kura huyo, zikiitaja kuwa ya kulazimisha na inayokwenda kinyume na sheria ya kimataifa.

Maeneo haya mapya yanayodaiwa kuingizwa ndani ya Urusi, pamoja na rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi mwaka 2014, ni asilimia 22 ya eneo zima la Ukraine.

Russland | Zeremonie zur Annexion ukrainischer Gebiete | Putin mit den Besatzungschefs
Rais Vladimir (katikati) na wakuu wa mikoa ya Ukraine iliyonyakuliwaPicha: Grigory Sysoyev/AP Photo/picture alliance

Sehemu ya Urusi milele na milele

Katika sherehe za kusaini mkataba wa muungano baina ya Urusi na maeneo hayo Ijumaa iliyopita, Rais Putin alisema kamwe Urusi haitayaachia kurudi kuwa sehemu ya Ukraine, licha ya kwamba Urusi ilisaini makubaliano ya Budapest ya mwaka 1994 ya kuitambua mipaka ya kimataifa ya Ukraine baada ya kuvunjia kwa uliokuwa Umoja wa Kisovieti.

Soma zaidi: Urusi yajiandaa kuyanyakua rasmi maeneo ya Ukraine

Hayo yanajiri wakati wanajeshi wa Ukraine wakiripotiwa kupiga hatua kubwa katika operesheni ya kuzikomboa sehemu zinazokaliwa na Urusi katika mkoa wa Kherson, wakivilazimisha vikosi vya Urusi kuzipa kisogo ngome ambazo wamezijenga tangu mwezi Machi.

Katika hotuba yake usiku wa kuamkia leo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema katika muda wa wiki moja tu, miji na vijiji vipatavyo 12 vimerejeshwa mikononi mwa Ukraine.

Ukraine Region Lyman ukrainische Soldaten
Mnamo wiki za hivi karibuni wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakiyakomboa maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wa UrusiPicha: Francisco Seco/AP Photo/picture alliance

Nchi za magharibi zaongeza shinikizo dhidi ya Urusi

Marekani imetangaza msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine, unaojumuisha mifumo minne ya makombora aina ya Himars, mizinga 32 pamoja na shehena kubwa ya vipuri na risasi, kwa azma ya kuviwahi vikosi vya msaada vitakavyotumwa na Urusi.

Soma zaidi:''Kura ya maoni" kukamilika kwenye maeneo ya Ukraine 

Afisa wa mkoa wa Kherson aliyewekwa na Urusi, Kirill Stremousov amesema leo kupitia shirika la habari la Urusi, TASS, kwamba wanajeshi wa Ukraine hawasongi mbele tena, na kuongeza kuwa vikosi vya Urusi vilikuwa vikijikusanya kuwarudisha nyuma.

Katika taarifa nyingine kuhusiana na mzozo huu, Jamhuri ya Czech ambayo ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya, imearifu kuwa umoja huo umekubaliana juu ya awamu ya vikwazo vipya dhidi ya Urusi, kuhusiana na hatua ya nchi hiyo ya hivi karibuni kuyanyakua maeneo ya Ukraine.

Vyanzo: rtre, afpe,ape