1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin anaaminika zaidi kuliko Trump

Sylvia Mwehozi
17 Agosti 2017

Utafiti mpya wa maoni uliochapishwa hivi karibuni unaonyesha rais wa Urusi Vladimir Putin anaaminika zaidi kuliko Donald Trump wa Marekani, hasa linapokuja suala la kushughulikia masuala ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/2iO8i
Kombobild Trump Putin

Utafiti uliochapishwa na kituo cha Pew ulilenga kupima mwitikio wa dunia kuhusu Urusi na kiongozi wake Vladimir Putin. Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kwamba mtu mmoja kati ya watu wanne katika nchi 37 kulikofanyika utafiti huo ana imani na rais wa Urusi kufanya jambo sahihi yanapokuja masuala ya kimataifa.

Washiriki kutoka Umoja wa Ulaya ndio walikuwa wakosoaji wakubwa karibu kwa asilimia 78 wakisema wanakosa uaminifu katika utawala wake. Utafiti huo, hata hivyo ulibainisha kwamba "licha ya imani kwa Putin katika kushughulikia masuala ya kimataifa ni ndogo kwa ujumla, lakini katika nchi nyingi anaaminika zaidi ukimlinganisha na rais Donald Trump."

Washiriki wa utafiti huo katika nchi kama vile Japan, Korea Kusini na mataifa saba ya Jumuiya ya kujihami ya NATO, Ugiriki, Ujerumani, Uturuki, Hungary, Ufaransa, Italia na Hispania, ambazo ni mshirika wa Marekani katika unngwaji mkono wa kijeshi na ulinzi, wote walielezea kumuamini zaidi Putin.

Sababu moja inayoweza kuwa imechagia haya ni maoni yasiyotabirika aliyotoa Bw. Trump katika masuala mbalimbali ya kidunia tangu aingie madarakni mwezi Januari, akihoji uhalali na ufanisi wa NATO, kuchelewesha uthibitisho wa makubaliano ya pamoja ya ulinzi na kuwatuhumu wanachama kwa kushindwa kuvuta kuonyesha uwezo wao.

Deutschland Hamburg - G20 - Donald Trump und Vladimir Putin
Donald Trump na Vladimir Putin wakati wa mkutano wa G20Picha: Reuters/C. Barria

Uungwaji mkono wa Putin dhidi ya Trump ulidhihirika zaidi Ugiriki na Ujerumani ambako amemshinda kwa pointi 31 na 14. Hapa Ujerumani, karibu robo ya washiriki walisema wanamuamini zaidi Putin.

Lakini sio raia wote katika nchi wanachama wa NATO ambao wanaonelea Putin ni kiongozi anayeaminika. Trump alipata uungwaji mkono zaidi nchini Uingereza, Canada, Uholanzi na Poland, kwa mujibu wa utafiti. Alionekana kuaminika zaidi kwa nchi zisizo mshirika wa NATO Australia na Ufilipino pamoja na Israel.

Pamoja na kuwa na mtazamo wa kiujumla wa Putin katika sera za kigeni, washiriki wachache wanafikiria Urusi kama kitisho cha usalama. Kwa ujumla asilimia 31 ya watu walielezea uwezo na ushawishi wa Urusi kama kitisho kikubwa katika nchi zao chini ya vitisho vingine kama vile kundi la itakadi kali la Dola la Kiislamu, mabadiliko ya tabia nchi na mashambulizi ya mtandaoani. Idadi hiyo hiyo pia iliifikiria China kama kitisho huku asilimia 35 ikionelea ushawishi wa Marekani kua ni hatari.

Maoni ya ukosoaji kuhusu Urusi yalitoka zaidi Ulaya na Marekani ambapo watu wengi walionysha wasiwasi namna serikali ya Urusi inavyoshughulikia uhuru wa kiraia na demokrasia. Ni Vietnam, Ugiriki na Ufilipino pekee ambao walikuwa na maoni ya kuunga mkono. Maoni yalitofautiana Mashariki ya Kati, Asia, Amerika ya Kusini na Afrika.

Matokeo hayo yametokana na utafiti uliofanywa na kituo cha Pew katika jumla ya nchi 37 duniani kote kati ya mwezi Februari na Mei.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DW

Mhariri: Bruce Amani