1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin amlaumu Rais wa Ukraine Petro Poroshenko

Admin.WagnerD1 Julai 2014

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema yeye pamoja na viongozi wa Ulaya walijaribu bila ya mafanikio kumshawishi rais wa Ukraine Petro Poroshenko kuurefusha muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine

https://p.dw.com/p/1CTzw
Picha: Reuters

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameagiza kurejea kwa operesheni ya kijeshi mashariki mwa nchi hiyo baada ya kutangaza jana usiku kuwa hatarefusha muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika eneo hilo na kusema waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo hilo hawakuyaheshimu makubaliano hayo.

Hatua hiyo ya rais wa Ukraine imekuja hata baada ya misururu ya mazungumzo kati yake na viongozi wa Ufaransa,Ujerumani na Urusi ambao walikubaliana kuwa kuna haja kuongezwa kwa muda wa makubaliano hayo kama sehemu ya kutafuta amani katika eneo hilo.

Poroshenko amejitwisha dahamana kisiasa na kijeshi

Putin amewaambia mabalozi wa Urusi waliokuwa wanakutana mjini Moscow kuwa Porosheno amechukua hatua ya kurejesha opresheni za kijeshi na hangeweza kushawishika kuwa amani ya kudumu haiwezi kupatikana kwa njia ya vita.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: Getty Images

Putin ameongeza kusema kuwa sasa Poroshenko kwa kuchukua uamuzi huo, amejitwisha dhamana kijeshi na kisiasa ya mzozo huo wa Ukraine.Kiongozi huyo wa Urusi ambaye amekuwa akishutumiwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kwa kuuchochea mzozo wa Ukraine amenukuliwa leo akiilaumu Marekani badala yake kuwa ndiyo inayouchochea mzozo huo kwa kuidharau Urusi.

Umoja wa Ulaya ulitarajiwa leo kuiwekea Urusi vikwazo zaidi vya kiuchumi lakini wanadipolomasia wakuu wa umoja huo walioukuwa wakikutana leo mjini Brussels wamesema hawatafanya hivyo mara moja kwasababu ya jinsi mambo yalivyo hivi sasa Ukraine kwani hawajapata sura kamili baada ya mapigano kati ya wanajeshi na waasi kuripotiwa kuzuka upya mashariki mwa Ukraine.

Umoja wa Ulaya wasita kuiwekea Urusi vikwazo

Hata hivyo wanadiplomasia hao wamesema wanaharakisha mchakato wa kuandika na kuorodhesha vikwazo hivyo vipya ambavyo huenda vikatangazwa wakati wowote.

Wanajeshi wa Ukraine wakishika doria katika eneo la Donetsk
Wanajeshi wa Ukraine wakishika doria katika eneo la DonetskPicha: picture-alliance/AP Photo

Mkutano uliofanyika wiki iliyopita wa viongozi wa nchi wanachama wa umoja wa Ulaya uliionya Urusi kuwa itawekewa vikwazo zaidi iwapo haitachukua hatua zaidi kuupunguza mzozo wa mashariki mwa Ukraine.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble amesema nchi yake haitaruhusu maslahi yake ya kibiashara kutatiza kutangazwa kwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi iwapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.

Kampuni za Ujerumani zimekuwa zikionya kuwa huenda zikapata hasara kubwa ya mabilioni ya euro iwapo Urusi itaongezewa vikwazo.Akizungumza na wanahabari hii leo mjini Berlin,Shaeuble amekiri kuwa kuiwekea Urusi vikwazo vipya kutaathiri biashara lakini baya zaidi ni kuruhusu sheria za kimataifa kukiukwa.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu