1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Puigdemont kusalia kizuizini Ujerumani

Sylvia Mwehozi
27 Machi 2018

Mahakama nchini Ujerumani imeendelea kumweka kizuizini kiongozi wa zamani wa jimbo la Catalonia, Carles Puigdemont, wakati akisubiri kurejeshwa Uhispania ili kukabiliana na mashitaka ya uasi.

https://p.dw.com/p/2v4ps
Belgien Carles Puigdemont
Picha: picture-alliance/dpa/AP/O. Matthys

Hayo yakijiri maandamano mapya yamezuia barabara kuu kadhaa katika mkoa huo wa Uhispania unaotaka kujitenga. 

Puigdemont ataendelea "kubaki kizuizini kwa hivi sasa, hadi uamuzi utakapotolewa juu ya mchakato wa kurejeshwa kwake", imesema mahakama ya kikanda ya Kiel, kaskazini mwa Ujerumani, ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi huyo kukamatwa.

Kukamatwa kwake hapa Ujerumani, kumeibua maandamano ya ghadhabu huko Catalonia na waandamanaji wamefunga barabara kuu kadhaa katika mkoa huo hii leo, ikiwemo kwa muda mfupi barabara kuu zinazounganisha Barcelona.

Spanien Katalonien Proteste
Vizuizi vilivyowekwa na waandamanaji Catalonia Picha: Getty Images/AFP/R. Roig

Puigdemont alikiimbilia uhamishoni miezi mitano iliyopita wakati waendesha mashitaka wa Uhispania walipojaribu kumshitaki kwa uasi katikati mwa jaribio lililoshindwa la Catalonia la kujitangazia uhuru mnano mwezi Oktoba mwaka uliopita. Alikamatwa siku ya jumapili baada ya kuvuka mpaka na kuingia Ujerumani akitokea Denmark, chini ya waranti ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa na Uhispania.

Kwamujibu wa wakili wake Jaume Alonso-Cuevillas, Puigdemont alikuwa njiani kurudi Ubelgiji, ambako anaishi uhamishoni baada ya mamlaka za Uhispania kuanzisha utawala wa moja kwa moja kwa jimbo la Catalonia. Mahakama ya Ujerumani imetupilia mbali ombi la timu ya mawakili ya kuachiliwa kwa kiongozi huyo, ikisubiri uamuzi wa kumrejesha nyumbani na mamlaka za Ujerumani. George Guentge ni mwendesha mashitaka wa jimbo la Schleswig-Holsteing la hapa Ujerumani na amesema "hii haimaniishi kwamba Puigdemont atarejeshwa nyumbani sasa, lakini kwamba sasa tupo katika mchakato sahihi wa kumrejesha. Tutaangalia ikiwa mchakato wa kumrejsha unakubalika. Sisi, kama ofisi ya mwanasheria mkuu, tunalishughulikia kutoka upande huu. Mahakama inayoamua ni mahakama kuu ya Schleswig."

Maandamano ya leo Jumanne yamerindima kwenye barabara za karibu na mpaka wa Ufaransa, pamoja na barabara nyingine inayounganisha Catalonia na pwani ya Uhispania ya kusini mashariki. Waandamanaji pia wamefunga barabara kuu inayoelekea katika mji wa Lleida, na barabara nyingine kati ya Tarragona na Valencia.

Pia maandamano hayo yamesababisha usumbufu mapema leo asubuhi kwenye barabara kadhaa za Barcelona, mji mkuu wa mkoa huo.

Spanien Katalonien Proteste
Polisi wakivunja vizuzizi vya waandamanajiPicha: Getty Images/AFP/R. Roig

Msemaji wa serikali ya Uhispania waziri Inigo Mendez de Vigo amesema kwamba hatma ya kiongozi huyo wa wanaotaka kujitenga iko mikononi mwa mahakama za Ujerumani, lakini akaelezea matumaini ya kurejeshwa kwake kwasababu Pugdemont "hashikiliwi kwa mawazo yake ya kisiasa".

Mendez de Vigo amewaeleza waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano wa baraza la mawaziri la Uhispania kuwa "hilo halikuwa suala la Uhispania".

Katika hatua ambayo imeshangiliwa na wafuasi wake, kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa imeandikisha madai ya Puigdemont kuwa Uhispania inakiuka haki zake za kisiasa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef