Puerto Rico yadai utaifa wa Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Puerto Rico yadai utaifa

Puerto Rico yadai utaifa wa Marekani

Gavana wa Puerto Rico anaapa kuifanya himaya hiyo ya Marekani kuwa jimbo la 51 la Marekani baada ya kura ya maoni kudai utaifa isiofungamanishwa kisheria kukumbwa na kususiwa na kujitokeza kwa idadi ndogo ya watu.

Gavana Ricardo Rossello amewaambia kundi la mamia kiasi ya watu waliokuwa wakipeperusha bendera za Marekani hapo Jumapili usiku kwamba hivi karibuni ataunda tume kuwateuwa maseneta wawili na wawakilishi watano kudai utaifa kutoka bunge la Marekani ambalo inabidi liidhinishe madai yoyote yale juu ya hadhi ya kisiasa ya kisiwa hicho.

Rossello amesikika akipiga makelele kwa umma huo kwamba "Marekani inabidi itii matakwa ya watu wetu" huku umma huo kiwa umezikumbatia bendera za Marekani na kucheza ngoma za kiashiria cha kudai utaifa.

Lakini wataalamu wanasema haiyumkini kwa bunge hilo la Marekani lenye kudhibitiwa na chama cha Republikan kukubali matokeo ya kura hiyo ya maoni ya Jumapili (11.06.2017) mbali na kukubaliana nao kwa sababu Puerto Rico inawapendelea chama cha Demokrat.

Msemaji wa rais wa Marekani Sean Spicer amesema hapo Jumaatatu kwamba mchakato huo unabidi upitie bunge la Marekani.Amesema "kwa vile hivi sasa watu wametamka huko Puerto Rico hili ni jambo ambalo bunge itabidi ilishihghulikie."

 

Zaidi ya nusu milioni wataka utaifa

Puerto Rico Gouverneur Ricardo Rossello (Reuters/A. Baez)

Gavana wa Puerto Rico Ricardo Rossello.

Zaidi ya watu nusu milioni wamepiga kura ya kuwa na utaifa wakati wa kura hiyo ya maoni ya Jumapili wakifuatiwa na 7,000 wakidai uhuru wa kujumuika/ na uhuru na wengine zaidi ya 6,800 wakitaka kuendelea kwa hadhi iliyonayo kisiwa hicho kwa hivi sasa. Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 23.

Hiyo ni idadi ndogo kabisa ya ushiriki katika uchaguzi wowote ule Puerto Rico tokea mwaka 1967 kwa mujibu wa Carlos Vargas wa Kituo cha Masomo ya Perto Rico katika Chuo cha Hunter kilioko New York.Ameliambia shirika la habari la AP hata miongoni mwa wapiga kura vijana ambao wameunga mkono kuwa na utaifa idadi iliojitokeza ni ndogo mwaka huu kwa kulinganishwa na kura za maoni zilizopita.Amesema "wafuasi wa utaifa imeonekana hawakuwa na hamasa juu ya kura hii ya maoni kama walivyokuwa miaka mitano iliopita."

Gavana Rosselllo ametupilia mbali wasi wasi huo kwa kusema kwamba kura hiyo  ya maoni ni mchakato wa demokrasia ambapo kwayo walio wengi husikilizwa wakati alipoulizwa kwa nini hawakujitokeza watu wengi kutetea mbadala wa utaifa.Pia amesema viwango vya ushiriki vinatofautiana kati ya asilimia saba na 35 kwa majimbo yakiwemo Wisconsin na Hawaii wakati yaliporidhiwa.

Vyama vitatu vya kisiasa Puerto Rico kikiwemo chama kikuu cha upinzani vimewataka wafuasi wao kususia kura hiyo ya maoni ambayo wameitangaza kuwa imeshindwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com