Poroshenko kutokomeza uasi Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Poroshenko kutokomeza uasi Ukraine

Rais Mteule Petro Poroshenko wa Ukraine ameapa kutokomeza uasi unaounga mkono Urusi mashariki mwa nchi hiyo. Kauli yake inakuja wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya wakiihimiza Urusi kushirikiana na rais mpya wa nchi hiyo.

Rais Mteule wa Ukraine Petro Poroshenko.

Rais Mteule wa Ukraine Petro Poroshenko.

Rais mteule Poroshenko ameliambia jarida la Ujerumani la Bild katika mahojiano yaliochapishwa leo hii kwamba watatokomeza kile walichokiita ugaidi kutokana na vita vinavyoendeshwa dhidi ya nchi yake.Poroshenko amesisitiza kwamba hatowi amri zozote zile kwa sababu bado hakuapishwa lakini amesema anawasiliana kwa karibu na serikali.

Amesema anaweza kusema hatimae operesheni hasa ya kijeshi imeanza na lengo ni kuwatia mbaroni viongozi wa waasi na kuwafungulia mashtaka.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele mjini Brussels wameitaka Urusi ishirikiane na Poroshenko na iendelee kuondowa vikosi vyake kwenye mpaka wake na Ukraine.Rasimu ya taarifa ya mkutano huo imesema Urusi inapaswa kutumia ushawishi wake kwa wapiganaji wanaotaka kujitenga ili kutuliza mzozo huo mashariki ya Ukraine.

Mapigano ya kuwania uwanja wa ndege wa Donetsk ambayo ni njia kuu ya usafiri kwa kitovu cha viwanda mashariki ya Ukraine yalizuka hapo Jumatatu baina ya vikosi vya serikali na waasi masaa machache tu baada ya rais mteule Poroshenko kuapa kuchukuwa hatua kali dhidi ya wale aliowaita magaidi.

Ukraine pia yashinikizwa

Mpiganaji muasi katika mji wa Donetsk.

Mpiganaji muasi katika mji wa Donetsk.

Wakati hofu ikiwa imetanda katika mitaa ya Donetsk, Rais Vladimir Putin wa Urusi ameitaka Ukraine kusitisha operesheni yake ya kijeshi katika eneo hilo la mashariki linaloshikiliwa na waasi ili kufanyike mazungumzo kati ya serikali ya Ukraine na waasi hao.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya pia wamemshinikiza Poroshenko juu ya haja ya kufanya kila juhudi kwa upande wake kupunguza mvutano wa mzozo huo na kuendelea kufanya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ili kuiweka Ukraine kwenye kanuni za Umoja wa Ulaya.

Rais Barack Obama wa Marekani amezunguza na rais huyo mteule na kumuunga mkono kikamilifu lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameitaka Ukraine kutumia njia za amani mahsusi kuurudisha udhibiti wake wa eneo la mashariki.

Waangalizi wa OSCE watoweka

Makao makuu ya Shirika la Usalama na Ushirikiano Ulaya (OSCE) Vienna,Austria.

Makao makuu ya Shirika la Usalama na Ushirikiano Ulaya (OSCE) Vienna,Austria.

Timu moja ya Shirika la Usalama na Ushirikiano OSCE barani Ulaya ya waangalizi wa kimataifa imenaswa kwenye mapigano ya Donietsk na kutoweka baada ya kushikiliwa kwenye kituo kimoja cha ukaguzi barabarani.

Shirika hilo la OSCE ambalo limetimiza dhima muhimu katika kujaribu kuumaliza mzozo huo limesema limepoteza mawasiliano tokea Jumatatu na waangalizi wake wanne akiwemo Mdanish,Mswisi, Muestonia na Mturuki wakati wakiwa kwenye doria mjini Donetsk.

Afisa wa OSCE aliyeko Vienna amesema waangalizi wao hao walikuwa wamezuiliwa katika kituo kimoja cha ukaguzi barabarani kabla ya kupoteza mawasliano nao wakati afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Ururuki amesema wamejulishwa kupitia njia zisizo rasmi kwamba waangalizi hao wako salama.

Mwandishi :Mohamed Dahman /AFP/dpa

Mhariri :Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com