1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nane wauawa katika maandamano DR Congo

Iddi Ssessanga
1 Januari 2018

Watu wanane wameuawa Juampili na dazeni kadhaa kukamatwa na vikosi vya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, wakati wa maandamano yalioitishwa na Kanisa Katoliki kumshinikiza rais Joseph Kabila aachie madaraka.

https://p.dw.com/p/2qAx2
Kongo Notre-Dame in Kinshasa
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Licha ya maombi, hasa kutoka kwa Umoja wa Mataifa kuheshimu haki ya raia kuandamana, wanajeshi walifyatua hewa ya kutoa machozi ndani ya makanisa na risasi za moto hewani kuvunja mikusanyiko ya waumini wa Kikatoliki, na katika kisa kimoja waliwakamata wavulana wanaohudumu kanisani kwa kuongoza maandamano mjini Kinshasa.

Mawasiliano ya intanet yalikuwa chini mnamo wakati makundi ya Kanisa na kisiasa yakikaidi amri iliyowekwa na serikali na kuendelea na maandamano hayo. "Vifo nane -- saba mjini Kinshasa na kimoja Kananga," katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, chanzo kutoka Umoja wa Mataifa kililiambiam shirika la habari la Ufaransa AFP, na kuongeza kuwa kulikuwepo na watu 82 waliokamatwa, wakiwemo mapadri, katika mji mkuu na 41 katika maeneo mengine ya nchi."

Kabila awaonya watakaofanya vurugu

Katika hotuba yake ya kumaliza mwaka, Kabila alisisitiza kuwa kutangazwa hivi karibuni kwa kalenda ya uchaguzi utakaofanyika Desemba 2018, "kunatupeleka pasina kurudi nyuma kuelekea kuandaliwa kwa uchaguzi".

Kongo Opposition
Waandamanaji wakishinikiza rais Joseph Kabilaaachie madaraka mjini Kinshasa.Picha: picture alliance/dpa/AP Photo/J. Bompengo

"Nawaalika mchukuwe jukumu (la mchakato wa uchaguzi) na mtekeleze haki yenu kupitia mchakato huu," aliongeza kusema katika hotuba hiyo iliyorekodiwa kabla na kutangazwa kupitia televisheni ya taifa.

Pia alionekana kutoa onyo kwa waandamanaji, akiwasihi raia kuchukuwa tahadhari ili "kuwazuwilia njia wale wanaotaka kutumia uchaguzi kama kisingizio katika miaka ya hivi karibuni, na ambao sasa wangejaribu kutumia vurugu, kuzuwia mchakato unaoendelea wa kidemokrasia kuitumbukiza nchi katika machafuko".

Msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo Florence Marchal alisema watu wasiopungua 82 wamekamatwa nchini kote kuhusiana na maandamano ya Jumapili. Alilaani matumizi ya nguvu dhidi ya maandamano ya amani na ukandamizaji wa haki.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Huma Rights Watch katika kanda ya Afrika ya Kati Ida Sawyer alisema vikosi vya usalama viliwapiga risasi na kuwauwa wanaume wawili nje ya Kanisa la Mt. Alphonse katika wilaya ya Matete.

Msemaji wa polisi ya Congo Kanali Pierrot Mwanamputu, hata hivyo, alisema wawili hao waliuawa baada ya kuzozana na polisi. Alisema askari wa polisi pia alifariki. Leonie Kandolo, msemaji wa mmoja ya makundi yalioandaa maandamano hayo, alisema zaidi ya watu 10 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Alisema pia kuwa wengine kadhaa, wakiwemo baadhi ya mapadri, wameweka kizuwizini.

Maandamano ya amani

Makanisa ya Kikatoliki na wanaharakati waliitisha maandamano ya amani baada ya ibada ya Jumapili, mwaka mmoja baada ya Kanisa Katoliki kusimamia utiaji saini wa makubaliano, yalioweka terehe mpya ya uchaguzi ili kupunguza mzozo katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Demokratischen Republik Kongo | Wahlkommision |  Corneille Nangaa
Mkuu wa tume ya uchaguzi ya DR Cngo Corneille Nangaa.Picha: DW/F. Quenum

Kabila ambaye muhula wake ulimalizika Desemba 2016, alikuwa amekubali kuitisha uchaguzi kufikia mwishoni mwa 2017. Tume ya Uchaguzi wa Congo inasema kura hiyo haiwezi kufanyika hadi Desemba 2018. Wakosoaji wanamtuhumu Kabila kwa kuahirisha uchaguzi ili kuendelea kusalia madarakani, na hivyo kusababisha wasiwasi kuongezeka na kuchochea vurugu na maandamano mabaya ya mitaani nchini kote tangu mwishoni mwa 2016.

Serikali ilikataa kutoa vibali kwa waandamaji siku ya Jumapili, na ilifunga mtandao wa intaneti na huduma za ujumbe mfupi nchini kote kabla ya maandamano hayo, kwa kile ilichosema ni sababu za kiuslama. Zaidi ya makanisa 160 yalishiriki katika maandamano hayo. Polisi ilijibu kwa kutumia gesi ya kutoa machozi katika baadhi ya maeneo ya mjini Kinshasa.

Tayari maandamano yalikuwa yametulia kufikia mchana, ingawa vizuwizi viliendelea kujengwa kuelekea sherehe za kuukaribisha mwaka mpya. Tume ya uchaguzi wa Congo imepanga tarehe mpya ya uchaguzi wa rais na bunge kuwa Desemba 23, 2018, ingawa upinzani umesema utakubaliana tu na ucheleweshwaji wa uchaguzi hadi Juni 2018.

Kabila anaweza kusalia madarakani hadi uchaguzi ujao utakapofanyika, ingawa anazuwiwa na katiba kuwania muhula mwingine. Taifa hilo halijawahi kuwa na makabidhiano ya amani ya madaraka tangu lilipopata uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape.