1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yafyatuwa mabomu ya kutowa machozi Kenya

10 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CneJ

NAIROBI

Polisi ya Kenya imefyetuwa mabomu ya kutowa machozi kutawanya zaidi ya wanawake 100 wafuasi wa upinzani waliokuwa wameandamana wakielekea kwenye kanisa katika mji mkuu wa Nairobi kufanya sala ya maombi kwa ajili ya amani kufuatia ghasia zilizozuka nchi nzima kutokana na uchaguzi tata wa rais.

Kamanda wa polisi David Kerini amesema waandamanaji hao hawakuijulisha polisi juu ya maandamano hayo na kwamba walipotakiwa watawanyike waligoma na kwa hiyo wakalazimika kutumia mabomu ya kutowa machozi.

Polisi imetawanya waandamanaji hao wakati Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais John Kofour wa Ghana akirefusha muda wa ziara yake nchini Kenya baada ya kushindwa kuleta usuluhishi kati ya upinzani na Rais Mwai Kibaki.

Kufour na mjumbe mwandamizi wa Marekani kwa Afrika Jendayi Frazer wamekuwa wakikutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Takriban watu 600 wameuwawa na wengine 260,000 wamepotezewa makaazi yao katika ghasia zilizozuka nchini kote ambazo kwa haraka ziligeuka kuwa visasi vya kikabila kufuatia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.