1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kenya yahimizwa kuchukua hatua dhidi ya wabakaji

Amina Mjahid14 Desemba 2017

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limetoa ripoti yake hii leo inayosema visa vingi vya unyanyasaji wa kingono vilijitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2017 nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/2pLuW
Kenia Oberstes Gericht annulliert Präsidentenwahl
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Ripoti hiyo iliyo na kurasa 31 iliyopewa jina"Walikuwa wanaume waliyovalia sare ya kijeshi, Unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana, katika uchaguzi wa Kenya mwaka 2017" inaangazia visa vibaya vya udhalilishaji wa kimwili, kiakili, kijamii na kiuchumi pamoja na uvunjifu mkubwa wa haki za binaadamu uliyofanyika wakati wa uchaguzi wa hivi karibuni.

Shirika hilo limegundua kuwa serikali ya Kenya ilishindwa kuwalinda raia wake dhidi ya visa hivi, kushindwa kuvichunguza ipasavyo, kutowachukulia hatua wahusika na kutohakikisha waathirika wanapata huduma bora na inayostahiki baada ya manyanyaso hayo.

Kenia Wahlwiederholung Ausschreitungen Sicherheitskräfte
Polisi wa Kenya katika eneo la Kawangware mjini NairobiPicha: Reuters/T. Mukoya

Katika kuandaa ripoti yake, shirika hilo la Human Rights Watch lilizungumza na wanawake 68, wanaume watatu ambao ni waathirika wa visa vya unyanyasaji wa kingono na watu 12 waliyoshuhudia visa hivyo katika maeneo ya Mathare Dandora na Kibera mjini Nairobi, Kisumu na Bungoma Magharibi mwa Kenya.

Shirika hilo pia lilizungumza na mashirika ya Kimataifa ya kiraia pamoja na yale ya nchini Kenya.

Wengi wa wanawake na wasichana waliohojiwa walitoa visa vya kusikitishwa vya kubakwa mbele ya familia zao, kuingizwa chupa, vyuma, magongo na uchafu mwengine katika sehemu zao za siri. Msichana mmoja alisemekana kuaga dunia mara baada ya kubakwa.

Shirika la Human Rights Watch lasema serikali imepuuzia visa hivi vinavyosemekana kufanywa na vikosi vya usalama. 

Purity Onyancha aliye na miaka 27 alijifungua tarehe 7 mwezi Agosti baadaye Agosti 11 alibakwa na maafisa watatu wa polisi. Alipohojiwa alisema anajihisi kama vile hana thamani tena, hazungumzi na watu anakosa usingizi na saa nyengine anafikiria hata kujitoa uhai wake.

Human Rights Watch Logo Symbolbild
Picha inayoonesha nembo ya shirika la Human Rights WatchPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Shirika la human Rights Watch linasema wengi wa waathirika hawajapokea huduma au matibabu baada ya kubakwa ikiwemo tembe za kuzuwiya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa na kuzuwia mimba.

Ripoti hiyo ya Human Rights watch inasema kizingiti cha kupokea huduma kama hizi kunatokana na unyanyapaa, kukosa huduma stahiki, kukosa taarifa ya kupata huduma ya haraka na mahali ambapo waathirika wa visa kama hivi wanaweza kwenda kupokea matibabu ya bure.

Aidha inadaiwa serikali ya kenya imepuuzia visa hivi vinavyosemekana kufanywa na vikosi vya usalama. Agnes Odhiambo mtafiti wa shirika la Human Rights watch amesema serikali inapaswa kubadilisha namna inavyosughulikia masuala ya unyanyasaji wa kingono na kuhakikisha wale wanaofanya visa hivi wanachukuliwa hatua kali na pia uwepo wa huduma ya haraka ya kuwapa waathiriwa ikiwemo ushauri.

Mwandishi : Amina Abubakar/Human Rights Watch 

Mhariri: Yusuf Saumu